ALLIANCE FC imefuzu hatua ya 32 ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC)
baada ya leo Jumamosi kuisambaratisha vikali Transit Camp mabao 3-1,mchezo ambao
umepigwa uwanja wa Nyamagana jijini hapa.
Licha ya mpira mwingi na wa kuvutia kwa timu zote lakini Alliance ilionyesha kitu cha ziada na
kufanikiwa kufuzu hatua hiyo huku wapinzani wakiyaaga rasmi mashindano hayo.
Alliance FC ndio walitangulia kupata bao likifungwa kwa ustadi kupitia Martin Kiggy
aliyepiga shuti kali akiwa nje ya 18 na kujaa wavuni.
Transti Camp ambao walikuwa wakipigiana mipira ya juu juu, walitulia na kufanya
mashambulizi na dakika ya 45 Idd Mbaga alisawazisha bao hilo na kwenda mapumziko
wakiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi lakini mbali na Transit kumiliki mpira zaidi, tatizo la kutumia
vyema nafasi pamoja na maamuzi ndani ya 18 iliwagharimu na kujikuta wakifungwa bao la pili
na la tatu dakika ya 55 na 65 kupitia David Richard.
Wakati huohuo, Gwambina FC wakiwa uwanja wao wa nyumbani wilayani Misungwi,
wameilaza Mbeya Kwanza mabao 3-0 na kufuzu hatua inayofuata.
Mabao mawili yaliyofungwa na Jacob Masawe na lingine walilojifunga Mbeya Kwanza
yameifanya timu hiyo ya mkoani Mbeya kuyaaga mashindano hayo.
0 Comments