YANGA imeanza vyema kampeni ya Kombe la FA baada ya leo Jumamosi kuichapa Iringa
United mabao 4-0 , mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ambapo watani wao Simba kesho Jumapili anacheza na AFC kwenye uwanja huo.
Ushindi wa Yanga ni ishara nzuri kwao kwenye michuano hiyo ambayo misimu miwili mfululizo watani zao wamekuwa wakitolewa hatua ya awali.Yanga walizitumia dakika 45 za kipindi cha kwanza kujihakikishia ushindi wakimaliza muda
huo wakiwa mbele mabao 3-0 yaliyowazima vijana wa Iringa United ambao kikosi chao
kilisheheni vijana wadogo.
Dakika 10 za kwanza tayari Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0 ambapo dakika ya saba
tu waliziamsha nyavu za wageni wao kwa bao safi la kichwa kilichopigwa na nahodha wa timu
hiyo Papy Tshishimbi akimalizia krosi safi ya kiungo Deuse Kaseke.
Dakika ya tisa Yanga waliongeza bao la pili likifungwa na winga Patrick Sibomana
aliyemalizia krosi safi ya beki Cleophas Sospeter ambayo iliachwa kidogo na mshambuliaji
David Molinga kabla ya mpira kumkuta mfungaji.
Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha Iringa na kuanza kupambana na dakika ya 18 almanusura
wapate bao kwa mpira mrefu wa adhabu lakini kipa wa Yanga, Farouk Shikhalo alikuwa
imara na kuupangua mpira kwa ufundi na kuwa kona iliyokosa madhara.
Yanga baada ya shambulizi hilo hawakuwa na haraka tena katika kutafuta mabao zaidi
wakicheza soka la pasi na kuwapa shida Iringa kuutafuta mpira.
Dakika ya 21, Iringa walimtoa Mohamed Mkumba aliyepata maumivu mapema wakati mpira
ukianza nafasi yake ilichukuliwa na Dayan Masue.
Dakika ya 38 Yanga walifanikiwa kupata bao la tatu likifungwa na na beki Lamine Moro
kwa kichwa safi akipokea mpira wa kona ya Sibomana na kuufanya mchezo huo kumaliza
dakika 45 za kwanza wakiwa mbele kwa mabao hayo.
Kipindi cha pili Yanga walirudi kwa kasi katika kupanua uongozi wao katika mchezo huo
ambapo dakika ya 50 winga mkongwe Mrisho Ngassa alipoteza nafasi nzuri kufunga kwa tik
tak mpira wake unakosa nguvu akipokea krosi safi ya Kaseke.
Dakika ya 53 mpira ulisimama kwa muda takribani dakika tano baada ya nyuki kuvamia
uwanjani na kuwafanya wachezaji kukimbia na kulala chini hali kadhalika mashabiki na
waamuzi.
Nyuki hao walianzia lango la Yanga hasa waliposimama mabeki wa kati na kuonekana
kumshambulia zaidi beki wa Yanga, Ally Sonso ambaye alitimua mbio na kukimbilia
vyumbani.
Hata hivyo baada ya dakika chache Sonso alirejea sambamba na wachezaji wengine watimu
zote na kuendelea na mchezo
Dakika ya 69 Yanga walifanikiwa kupata bao la nne likifungwa na Molinga aliyeunasa
mpira uliachwa nyuma na Sibomana kisha kumpiga chenga kipa wa Iringa Nelson Emmanuel
kisha kuuweka wavuni.
Kabla ya bao hilo Yanga walionyesha ukomavu wakigongeana vyema mpaka wakafanikiwa
kupata bao hilo.
Mpaka mwisho wa mchezo Yanga waliibuka na ushindi huo wa mabao 4-0 na kusonga mbele
hatua inayofuata.
0 Comments