Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amewataka waalimu wote wa michezo mbalimbali kujiunga na Chuo cha Michezo Malya kilichopo Jijini Mwanza ili kupata mafunzo ya muda mrefu na mfupi yanayotolewa chuoni hapo kwa lengo la kupata utaalamu mzuri wa kufundisha michezo hapa nchini.
Shonza ameyasema hayo Mkoani Morogoro wakati alipofungua mashindano ya mpira wa Wavu kitaifa ambapo amesema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI zinashirikiana katika kukuza michezo hapa nchini ikiwemo kuhamasisha walimu wa michezo kuongeza ujuzi unaoendana na wakati katika kufundisha michezo.
“Wizara yetu kupitia Chuo cha Michezo Malya inatoa mafunzo ya cheti pamoja na astashahada kwa waalimu wa michezo na wanapomaliza wanakwenda kufundisha michezo katika shule zetu na kwa wanamichezo, hivyo nitoe rai kwa waamuzi pamoja na waalimu ambao hamjapata mafunzo hayo mjiunge na chuo hicho ili kupata ujuzi zaidi wa kufundisha michezo”alisema Shonza.
Aidha Shonza ameupongeza uongozi wa Shirikisho la mpira wa Wavu hapa nchini (TAVA) kwa jitihada kubwa uliofanya mpaka kufanikisha ushiriki wa timu za Taifa za Wavu wa ufukweni katika michuano ya Afrika iliyofanyika katika nchi za Kenya,Algeria,Misri pamoja na Cape verde ambapo zimeiletea heshima na kuitangaza vyema nchi.
Vilevile Shonza ameihakikishia TAVA pamoja na Vyama vya Michezo vyote hapa nchini kuwa Wizara itaendelea kutoa ushirikiano kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI kushiriki katika mashindano ya UMITASHUNTA NA UMISETA kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Taifa.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA) Bw.Benedito Kambanyuma amesema kuwa michuano ya klabu bingwa ya Taifa kwa wanaume na wanawake hufanyika kila mwaka tangu mwaka 2018 ambapo ilianzishwa ligi kupitia vyama vya Mikoa na washindi wanne wa kila mkoa hukutana katika michuano na kupata bingwa wa Taifa.
0 Comments