Aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ((TFF), Jamal Malinzi na wenzake watatu wameonekana hawana kesi ya kujibu katika mashtaka 10 kati ya 30 yaliyokuwa yakiwakabili.
Washtakiwa hao wanne wamebakiwa na mashtaka 20 wanayotakiwa kujitetea huku mshtakiwa watano Miriam Zayumba akiachiwa huru baada ya kuonekana hana kesi ya kujibu kwa mashtaka yote yaliyokuwa yakimkabili.
Uamuzi huo umetolewa Jumanne hii, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vilivyotolewa na Jamhuri.
Hakimu Kasonde amesema mashtaka ambayo washtakiwa wameonakana hawana kesi ya kujibu, upande wa Jamhuri umeshindwa kuonesha kama washtakiwa wana kesi ya kujitetea.
Mahakama iliwafahamisha haki zao washtakiwa kwamba wanaruhusiwa kujitetea wenyewe kwa kiapo ama kuita mtu yoyote kama mashahidi wao.
Pia walifahamishwa kwamba wanayohaki ya kunyamaza kimya lakini kwa kufanya hivyo mahakama itaamini kwamba ushahidi uliotolewa na Jamhuri ni sahihi.
Washtakiwa walikubali kujitetea kwa kiapo na watakuwa na mashahidi ambapo wataanza kujitetea Agosti 6 mwaka huu.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Katibu wa shirikisho hilo, Selestine Mwesigwa na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 20 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017. Ambapo Meneja wa Ofisi TFF, Miriam Zayumba ameachiwa huru.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali yakiwamo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa dola za Marekani 173,335.
0 Comments