Naibu Waziri, Jumaa Aweso, ametoa onyo kwa Jumuiya zote za Watumia Maji zenye tabia ya ubadhirifu wa fedha kuwa zitafutwa kwa kuwa zinaenda kinyume na malengo ya uundwaji, ambayo kimsingi ni uendeshaji wa miradi ya maji kwa faida na kudumu kwa muda mrefu.
Aweso ametoa onyo hilo mara baada ya kupokea taarifa ya Jumuiya ya Watumia Maji ya Mradi wa Maji Uyovu (JUWAMAU) na kubaini ina kiasi cha Shilingi milioni 145 zilizohifadhiwa benki na kufurahishwa na uendeshaji mzuri wa mradi huo.
Akisema kuwa kuna haja ya kuwa na mabadiliko sanjari na ujenzi wa miradi usimamizi wa ukaribu jumuiya hizo ni muhimu sana kama tunataka miradi yetu iweze kujiendesha vizuri na kukidhi mahitaji ya huduma ya maji kwa wananchi vijijini.
Ameendelea kusema kuwa JUWAMAU ni ya mfano wa kipekee, na kutoa pongezi kwa uongozi wake. Akiahidi kutoa fursa ya kuwajengea zaidi uwezo na kutoa msaada wa rasilimali fedha waweze kuongeza wigo wa huduma kwa Mradi wa Uyovu kufika maeneo mengi zaidi.
Aweso amekiri kuwa kumekuwa na tatizo katika usimamizi wa miradi ya maji kwa jumuiya nyingi za maji, yanayo ambatana na matumizi mabaya ya fedha zinazotokana na mauzo ya maji iliyotakiwa kutumika kwa maendeleo ya miradi na kuchangiaa miradi mingi kutokuwa endelevu.
Akitoa ufafanuzi zaidi amesema baada ya kutambua mapungufu hayo Wizara ya Maji kupitia Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imebadili mfumo wa uendeshaji kwa lengo la kuimarisha jumuiya hizo ikuhusisha kigezo cha taaluma kwa nafasi ya Mwenyekiti na Mhasibu.
Naibu Waziri Aweso amesema Bukombe ni moja ya Halmashauri zitakazopewa kipaumbele kutokana na kutoridhishwa na hali ya upatikanaji wa maji na miradi mingi kutokamilika, na hata iliyokamilika bado hainufaishi wananchi.
0 Comments