Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka wizara ya Maliasili na Utalii kutenganisha eneo la uwindaji Selou (Hunting block) kwa kutengeneza Hifadhi ya Taifa ambayo itaitwa Hifadhi ya taifa ya Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji mkoani Pwani utakaozalisha megawatt 2,115, Rais Magufuli amesema kuwa eneo la uwindaji la Selou ni eneo ambalo limezunguka mradi huo mkubwa wa umeme na lina urefu wa kilomita za mraba elfu 57.
"Eneo la Selou ni eneo kubwa ambalo linachukua takribani kilomita 50, hivyo ni lazima Wizara itenge eneo ambalo litatengenezwa na kuwa Hifadhi kuweza kukidhi mahitaji ya utalii na kukisaidia kizazi kijacho kuendelea kuenzi mambo ambayo ameyafanya baba wa Taifa,” amesema Rais Magufuli.
Amesema maeneo ya uwindaji wa wanyama yanafikia 47 katika mbuga ya wanayama Selou hivyo Wizara ya Maliasili lazima itenge eneo la hifadhi na la uwindaji, ili kuimarisha utalii na kuvutia watalii wengi katika mbuga hiyo
Rais Magufuli alisisitiza kuwepo kwa utaratibu kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia maeneno ambayo yanavitalu wa uwindaji ili kuhakikisha kuwa Serikali inafaidika na maeneno hayo, pia aliagiza barabara ya kutoka Fuga kilomita 60 kwenda mahari ambapo mradi unajengwa ianze kutengenezwa kwa rami ili kufungua sekta ya utalii katika Mbuga ya wanayama Selous.
Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji ni mradi ambao unaweza kudumu kwa muda wa miaka 60 ambapo utasaidia kuzalisha umeme wa kutosha na kusaidia Tanzania kuweza kutekeleza malengo ya milenia ya maendeleo endelevu.
Amesema mradi wa mto Rufiji utasaidia kuchochea maendeleo katika sekta ya viwanda ambapo wewekezaji wataweza kupata umeme wa uhakika na kwa bei nafuu na wenye kuaminika ili kuweza kuzarisha bidhaa zenye ubora.
“Mradi huu wa umeme wa mto Rufiji unaweza kudumu kwa muda wa miaka 60 na kusaidia watanzania kupata umeme wa uhakika na wenye gharama nafuu ambao utasaidia wawekezaji kupata huduma ya umeme kwa uhakika bila mgao ili kuweza kuzarisha bidhaa zenye ubora na kuweza ushindano kwenye masoko mbalimbali ya kimataifa,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisisitiza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, mkandarasi anatakiwa kutumia wafanyakazi walioko karibu kwa kazi ambazo siyo za kitaalamu, akasisitiza ajira zitolewe kwa wenyeji wa maeneo ya mradi kwa mikoa ya Morogoro na Pwani, na amewataka wananchi kuchangamkia fursa kwa miezi hiyo 36 ya ujenzi.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema kuwa Ndoto ya Rais Magufuli ya kuenzi mambo makubwa ya Baba wa Taifa, Mwl.Julias Nyerere ikiwemo utekelezaji wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme katika maporomoko ya maji ya mto Rufiji.
“Mhe. Rais, ndoto yako leo imeanza kupata mafanikio, ndoto yako ni kupeleka umeme hadi kule kijijini kwa wananchi wa kawaida na umetoa agizo kuwa kila nyumba ya mtanzania iwe ya bati, nyasi au tembe lazima iwake umeme, kwa hiyo umeme huu ambao ujenzi wake umezinduliwa leo ni kukamilisha azma yako bila kujali maisha ya watanzania”, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
0 Comments