Serikali kupitia Wizara ya Afya Zanzibar imeahidi kushirikiana na sekta mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha inafikia lengo la kuondoa Homa ya Ini Zanzibar ifikapo mwaka 2030.
Hayo aliyasema Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed huko katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazi Mmoja wakati wa maadhimisho ya siku ya homa ya ini duniani ambayo hufanyika kila ifikapo Julai 28 ya kila mwaka .
Amesema Serikali imepanga mikakati kuweza kudhibiti homa hiyo kwa kuwapatia matibabu ya chanjo wenye mahitaji maalum ikiwemo wauguzi ambao wanawahudumia wagonjwa mbali mbali ili waweze kujiepusha na maambukizi.
Amesema ugonjwa wa homa ya ini imeenea sana duniani kote hasa Bara la Afrika na zaidi kwenye nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara ikiwemo Zanzibar takwimu za mwaka 2015 zinaonyesha wastani wa watu milioni 257 wanaishi na maambukizi ya homa ya ini B na milioni 71 ya homa ya ini C duniani na vile vile watu karibu milioni 1.4 hufa kila mwaka kutokana na madhara ya maradhi hayo .
Ameeleza ripoti za utafiti maalum wa kutathmini hali halisi ya homa ya ini bado haujafanyika Zanzibar ambapo takwimu zinathibitisha uwepo wa maambukizi ya homa ya ini inaonyesha walioathirika zaidi na ugonjwa huo ni watu wa makundi maalum (key population )ambao wamefikia asilimia 2-6 kwa homa ya ini B na asilimia 1-25 ya homa ya ini C.
Alifahamisha miongoni mwa watu waliopimwa kwa ajili ya kuchangia damu kwa hiyari katika mwaka 2011 -2016 walionekana kuambukizwa ya homa ya ini B ni asilimia 2.4 na ini C asilimia 0.4
Waziri Hamadi amesema anza ya Serikali kuwapa huduma wananchi wake wote bila ya ubaguzi kwa lengo la kuwanusuru kutokana na madhara pamoja na vifo vinavyoweza kusababishwa na homa ya ini .
Aidha alisema Wizara ya Afya imeunda kitengo maalumu cha huduma ya homa hiyo ili kupanga kuongoza na kusimamia utekelezaji wa huduma ya homa ya ini katika ngazi ya taifa wilaya vituo vya afya na jamiii
Alieleza tayari Wizara imeanza kutoa elimu kuhusu homa ya ini katika ngazi zote za huduma ya afya ili kuengeza uelewa pamoja na kuhamasisha kinga kwa wafanyakazi ili kutoa ushauri na msaada wa kitaalamu katika mapambano dhidi ya homa ya ini .
Kauli mbio ya mwaka huu ni 'WEKEZA KATIKA KUONDOA HOMA YA INI ZANZIBAR'.
Mapema Waziri wa Afya Hamadi Rashid Mohamed alizindua chanjo ya homa ya ini kwa wafanyakazi wa hospitali ya mnazi mmoja na kuwataka wafanyakazi hao kujikinga kwa chanjo hiyo
Hata hivyo aliwataka wauguzi kufuata maadili ya kikazi kwa kutotoa taarifa za wagonjwa wanaowapatia tiba pale wanapofika hospitalini hapo kwa matibabu
Alisema homa hii imeanza kuiathiri jamii hivyo mkakati wa pamoja unahitajika kwa kuweza kuutokomeza kwa kutumia chanjo na masharti yaliyowekwa
Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Dk Marijani Msafiri alisema zoezi la chanjo kwa wafanyakazi ni muhimu kwani maradhi hutoka kwa mgonjwa kuja kwa muunguzi
Alisema chanjo zilizopo zitakidhi kwa wafanyakazi wa hospitali ya mnazi mmoja hivyo aliwataka wauguzi kuendelea na zoezi hilo ili kufikia malengo ya serikali kwani ugonjwa huu maambukizi yake huwa kama ya virusi vinavyosababisha ukimwi .
0 Comments