Windows

Simba aikalia Mbao Morogoro

Kikosi cha Simba kimeibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya kikosi cha Mbao kutoka jijini Mwanza katika mchezo uliofanyika Morogoro katika uwanja wa Jamhuri ikiwa ni mwendelezo wa ligi kuu Tanzania bara.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha mechi 10 bila kupoteza wala kutoka sare ikijumuisha michezo ya ligi kuu pamoja na ligi ya mabingwa Afrika licha ya kuendelea kushika nafasi ya tatu kwenye TPL.

Nahodha John Raphael Bocco ameibuka kuwa shujaa baada ya kufunga magoli mawili, goli la kwanza alitupia kimiani dakika ya 25 baada ya krosi ya Mohammed Hussein, goli la pili kwa penati dakika ya 59.

Meddie Kagere amekwamisha wavuni goli la 14 la msimu upande wake huku likiwa goli la tatu kwa upande wa Simba katika dakika ya 80 ya mchezo kwa njia ya penati baada ya kuangushwa kwenye kisanduku na mlinzi wa Mbao David Mwasa.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha alama 57 kwenye michezo 22 katika nafasi ya 3 wakati ambapo Mbao FC jahazi linazidi kuzama ikiwa na alama 36 michezo 31 kipindi ambacho timu ipo kwenye mikono ya kocha mpya Mayanga baada ya Ally Bushiri kutimuliwa.

Kinara wa ligi hiyo ni Yanga yenye alama 67 kwenye michezo 28 na Azam FC nafasi ya pili kwa alama 59 michezo 28 pia.

Aidha, kuisha kwa mtanange huo Simba inaanza kujiandaa na mchezo wa mkondo wa kwanza wa ligi ya mabingwa Afrika hatua ya robo fainali dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Mchezo utakaofanyika dimba la taifa April 6.


Post a Comment

0 Comments