Windows

Liverpool yarejea kileleni kupitia bao la kujifunga Tottenham

Bao la dakika ya misho la Toby Alderweireld liliipa Liverpool ushindi wenye thamani isiyokuwa na kipimo na kuwarejesha kileleni mwa ligi ya Premier. Baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa, uwanja wa Anfield ukalipuka kwa shangwe na vifijo kuthibitisha kuwa Liverpool walipata ushindi wa 2 – 1 dhidi ya Tottenham Hotspur. Wageni Spurs walionekana kuwa wanaelekea kuponyoka na pointi moja – na hata wakapoteza nafasi kochokocho cha kuwa kifua mbele katika mechi hiyo – baada ya Lucas Moura kuisawazisha bao la kipindi cha kwanza la Liverpool kwa njia ya kichwa lake Roberto Firmino.

Liverpool walikuwa ukingoni mwa kujikuta nyuma ya vinara Manchester City ambao walishinda 2 – 0 dhidi ya Fulham Jumamosi, hadi pale kinyanganyiro cha ubingwa wa ligi kilichukua mkondo tofauti katika dakika za mwisho mwisho za mchezo.

The Reds sasa wanangoza ligi na mwanya wa pointi mbili mbele ya City lakini wamecheza mechi moja zaidi.

Katika mechi ya mapema, Chelsea waliponea chupuchupu baada ya kutoka nyuma na kupata ushindi wenye utata ugenini dhidi ya Cardiff City wanaopambana kukwepa kushuka ngazi. Ushindi huo ulipunguza shinikizo dhidi ya kocha Maurizio Sarri.

Cardif waliwazuia Chelsea na kipindi cha kwanza kikaisha kwa sare tasa licha ya Chelsea kuudhibiti mpira. Wenyeji walipata bao dakika moja baada ya kipindi cha pili kuanza kupitia kwa Kombora safi la Camarasa. Mashabiki wa Chelsea wakaanza kuimba nyimbo za kumtaka Sarri atimuliwe.

Zikiwa zimesalia dakika tano mchezo kumalizika, Ceaser Azpilicueta alisawazisha akiwa katika nafasi ya kutotea na kisha katka dakika ya majeruhi mchezaji aliyeingia kama nguvu mpya Ruben Loftus Cheek alipiga kichwa wazuni na kuivunja mioyo ya Cardiff.


Post a Comment

0 Comments