Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier amefurahishwa na huduma zinazotolewa katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi cha Muhimbili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu mapema wakati wa kukagua na kufuatilia maendeleo ya ushirikiano kati ya nchi ya Ufaransa na Tanzania katika masuala ya utafiti mafunzo na utoaji wa huduma za Afya katika chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Muhimbili.
Kwa kiasi kikubwa Waziri Ummy pamoja na Balozi huyo wameridhishwa kwa kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Wataalamu katika chuo hicho ikiwemo utafiti, mafunzo na utoaji wa huduma za afya.
“Binafsi tumeridhishwa na kazi kubwa na nzuri zinazofanywa na wataalamu wetu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi cha Muhimbili, katika masuala ya utafiti tumeona kazi kubwa inayofanyika katika utafiti juu ya dawa za kuua wadudu”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema hakuna sheria nzuri za udhibiti wa dawa hizi nchini hivyo Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Muhimbili na Serikali ya Ufaransa itaendelea kufanya utafiti na kuona jinsi gani itapunguza madhara ya utumiaji wa dawa za kuua wadudu kwa binadamu.
Pamoja na hayo, Waziri Ummy amefurahi kuona ushirikiano ambao Serikali ya Ufaransa inaendelea kuutoa katika huduma za watu wenye tatizo la Seli nundu “Sickle Cell”.
“kwa Mujibu wa Tafiti tuna jumla ya watu 200,000 nchini ambao wana tatizo la seli nundu na watoto ambao wanazaliwa ni 11,000 kwahiyo tumejadiliana na Serikali ya Ufaransa kuona ni jinsi gani tunaweza kuboresha huduma za ugunduzi ili tuweze kuwatambua mapema watoto pale wanapozaliwa na tatizo hili na kuhakikisha huduma za matibabu zinapatikana ikiwepo dawa ya kupunguza maumivu inapatikana”. Amesema Waziri Ummy.
Kufuatia hatua hiyo Waziri Ummy amemuomba Balozi Frederic kushawishi makampuni makubwa ya kutengeneza dawa kutoka Ufaransa yaweze kusaidia katika kuzalisha dawa ya kupunguza maumivu ya Seli nundu inapatikana kwa Watanzania wengi.
0 Comments