Windows

Ajibu, Mkude Wanogesha Mazoezi Stars

 WACHEZAJI nyota wa Klabu ya Simba wakiongozwa na John Bocco, Ibrahim Ajibu na Jonas Mkude ambao walikuwa nchini Afrika Kusini jana, walinogesha mazoezi ya Taifa Stars baada ya kufanya kwa mara ya kwanza. Wachezaji hao hawakuwa wameripoti katika timu hiyo ambayo inajiandaa kucheza na Kenya katika mechi ya michuano ya Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (Chan).

 

Ajibu na Mkude hawakuitwa katika kikosi cha kocha Emmanuel Amunike kilichoboronga Afcon kule Misri, na jana walikuwa kivutio kikubwa walipoonekana mazoezini. Nje ya Bocco, Mkude na Ajibu wachezaji wengine wa Simba waliowasili ni Aishi Manula, Gadiel Michael, Hassan Dilunga na Erasto Nyoni.

Kaimu kocha mkuu wa Stars, Ettiene Ndayiragije amesema: “Wachezaji hawa wa Simba wameingia na wako vizuri, nimewaona wakifanya vizuri na tunaendelea kuwajenga ili tushinde mechi hiyo.

 

“Hii ni nafasi yetu sisi kulipiza kisasi kwao baada ya kupoteza kule Misri ambapo tulipotea kidogo tu, ninaamini kwamba kwa jinsi tulivyo, basi tutafanya vizuri mechi hiyo.”

 

“Hadi sasa mchezaji Mudathir Yahya hatakuwepo kwa sababu hajafanya mazoezi na wenzake na bado ana maumivu, lakini wengine wote wapo vizuri kwa ajili ya mechi hiyo.” Stars itavaana na Kenya Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar kabla ya marudiano Agosti 4 nchini humo.

SWEETBERT LUKONGE NA SAID ALLY, Dar

The post Ajibu, Mkude Wanogesha Mazoezi Stars appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments