Windows

SEVILLA: TUMEKUJA KUCHEZA NA MABINGWA

RAIS wa Klabu ya Sevilla kutoka Hispania, Jose Castro, amesema wamekuja nchini kucheza na Simba ambao juzi wametetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki ulioandaliwa na SportPesa. 
Mchezo huo unaotambulika kama ‘La Liga World SportPesa Challenge’ kati ya Sevilla dhidi ya Simba, utachezwa leo usiku Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na kuonyeshwa na DSTV kupitia chaneli ya SuperSport 9.  
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Castro alisema walifurahia mapokezi waliyopata juzi usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. 
“Tumepata taarifa kwamba tunaokutana nao jana (juzi) wamekuwa mabingwa wa ligi kwa mara ya 20, hivyo tunachukua fursa hii kuwapongeza sana,” alisema. 
Castro alisema, ziara ya mabingwa hao mara tano michuano ya Europa League chini ya udhamini wa SportPesa, itasaidia kukuza soka la Tanzania. 
Naye Rais wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Wallace Karia, aliwakaribisha Sevilla na kuwatakia mchezo mwema dhidi ya Simba.
Aidha, Karia aliwashukuru SportPesa kwa kufanikisha ziara ya Sevilla na shughuli zote zinazohusu soka watakazofanya wakiwa nchini ikiwemo mchezo wa leo. 
Alisema kuikaribisha timu kubwa kama Sevilla, itasaidia kuweka rekodi nzuri katika soka la Tanzania.
“Tunawakaribisha sana na mjiandae kwa sababu mpira utakaochezwa sio wa kitoto,” alisema Karia. 
Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas, naye kwa upande wake alisema wanajivunia kuwa wadau wa kweli wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini na kuwaomba mashabiki wa soka kujaa uwanjani.
Tarimba alisema wameweka viingilio vya Sh 5,000 na Sh15,000 ili kuwavutia mashabiki na kuujaza uwanja huo na kwamba, tiketi hizo zinapatikana kwa mawakala wa Selcom na vituo vya mafuta vya Puma.

Post a Comment

0 Comments