Windows

Aussems: Nyie njooni muone soka


SIMBA ikiwa ndio kwanza imetoka kutetea taji lake la ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa pili mfululizo mchana wa jana Jumatano ilirejea jijini Dar kutoka Singida, ikipitia Dodoma na usiku wa leo itakuwa Uwanja wa Taifa, kukinukisha na Sevilla.


Mabingwa hao watavaana na Sevilla kutoka Hispania katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ambapo mshindi atanyakua kikombe, jambo lililompa mzuka Kocha Patrick Aussems na kuamua kuwaita mashabiki wa Msimbazi kwenda uwanjani kupata burudani toka kwao.


Aussems na vijana wake walitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JKNIA saa 6:30 mchana na kusisitiza licha ya uchovu wa kucheza mfululizo, lakini bado wataionyesha soka Sevilla kwani wanataka heshima mbele ya Wahispania hao.


Wachezaji 18 wa Simba walipewa ruhusa ya saa 1 kwenda kupumzika majumbani, lakini wakatakiwa usiku wa jana Jumatano wote kuwepo kambini katika hoteli ya Sea Scape kwa maandalizi ya mchezo wa leo utakaopigwa saa 1:00 usiku.


Kocha Aussems amewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi ili kuendeleza shangwe na sherehe za kuchukua ubingwa wa ligi msimu huu kwa kuiduwaza Sevilla.


“Tutaingia katika mchezo huo kwa kucheza zaidi soka la kuvutia ili mashabiki wetu watakaojitokeza uwanjani wapate nafasi ya kufurahi kama timu yao ilivyotoka kuchukua ubingwa ambao ulikuwa malengo yetu makuu kabla ya kuanza kwa msimu huu,” alisema.


Mbali na mchezo huo, Aussems aliweka mipango yake hadharani kuelekea msimu ujao na kusema Simba itafanya mambo ya msingi ikiwemo usajili wa wachezaji wa maana kulingana na mapungufu aliyoyaona msimu huu ili kuwa imara zaidi.


“Katika msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika tuliishia katika hatua ya robo fainali, Ligi Kuu Bara tumefanikiwa kutwaa tena ubingwa, lakini katika mashindano mengine ya ndani yote tumeshindwa kufanya vizuri licha ya Kombe la Mapinduzi na Kagame kucheza fainali na zote tulipoteza,” alisema Aussems na kuongeza:


“Mafanikio ya msimu huu yameshapita kubwa niwapongeze wachezaji wangu kwa namna walivyopambana kwa hali na mali mpaka kufanikisha malengo hayo lakini bila kusahau viongozi, wanachama na mashabiki wote ambapo timu ilipo na wao walikuwepo.”


Aidha Aussems alisema walipofikia msimu huu ndio mwanzo wa malengo ya msimu ujao kama kutwaa ubingwa wa ligi utakaowapa nafasi ya ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika, akisisitiza wanataka kufika mbali zaidi, lakini pia kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano ya ndani ambayo kwa msimu huu walichemsha.


“Kimsingi msimu huu nilikuwa na timu bora katika kila maeneo kwani washambuliaji wangu wote waliweka rekodi mbalimbali za kufunga ambazo kama si ubora wa sehemu ya kiungo na sehemu ya ulinze pengine lisingewezekana hilo kwa maana hiyo wote walikuwa bora na kufanya kazi kufanikiwa,” alisema Aussems.


KUKUTANA NA MO


Katika hatua nyingine Aussems alisema anatarajia kukutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ kwa ajili ya kujadili hatma yake ya kubaki Simba na masuala yote ya usajili wa wachezaji wapya na wale ambao wataachana nao.


Mwanaspoti lilikufichulia Aussems ataendelea kukinoa kikosi cha Simba msimu mmoja lakini mkataba utakuwa na malengo zaidi ya yale ambayo walikubaliana msimu huu unaomalizika uliokuwa na malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi na kufika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.


“Tutakutana baada ya ligi kumalizika kabla ya kwenda likizo nyumbani, ila ninaamini kila kitu kitakwenda sawa katika suala la mkataba wangu na kufanya usajili wa nguvu.”


Simba imebakisha michezo miwili ya Ligi Kuu dhidi ya Biashara ya Musoma jijini Dar na Mtibwa Sugar utakaochezwa Moro.


Post a Comment

0 Comments