

PESA ni sabuni ya roho asikwambie mtu. Hii ni kutokana na mabosi wa Yanga kuahidi kumpa mkataba mpya mnono nahodha wa timu hiyo, Ibrahim Ajib, ili msimu ujao waendelee kuwa naye.
Hatua hiyo ya Wanajangwani inakuja baada ya Klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Simba kuonyesha nia ya kumhitaji nyota huyo mkali wa pasi za mwisho za mabao.
Mazembe na Simba zimeingia vitani kuisaka kwa udi na uvumba saini ya Ajib ambaye amekuwa na msimu mzuri akiwa na kikosi cha Yanga kutokana na mabao yake ya ‘kideo’ na pasi za mwisho.
Japokuwa Yanga imeambulia patupu msimu huu, lakini Ajib ni miongoni mwa nyota waliofanya vizuri katika msimu unaoelekea ukingoni.
Yanga ilikuwa haipewi nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kutokana na klabu hiyo kuyumba kiuchumi, lakini pia aina ya usajili walioufanya kabla ya kupata viongozi wapya.
Moja ya mabao yake ya ‘kideoni’ ya kukumbukwa ni lile alilolifunga katika mchezo dhidi ya Mbao FC uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, baada ya kuunganisha mpira uliookolewa na mabeki.
Mashabiki wa soka walilifananisha bao hilo na lile alilowahi kulifunga Zlatan Ibrahimovic alipokuwa akiichezea Sweden.
Kwa utulivu wa hali ya juu, kiungo huyo alibinjuka na kuupiga mpira katika staili ya tiktaka na kumshinda kipa Hashim Mussa na kutinga kimiani.
Akizungumza na BINGWA, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, amekiri klabu hiyo kupokea ofa kutoka Mazembe na Simba zikimhitaji Ajib.
“Kimsingi Mazembe wameleta ofa ya Dola za Marekani 25,000 (sawa na Sh milioni 57) fedha ambazo akiwa hapa Yanga anaweza kuzipata, Simba wenyewe nao walikuwa tayari kumpa Sh milioni 30, kwa hiyo tumekaa na kushauriana tumeona uwezo wa kumbakiza tunao,’’ alisema Mwakalebela.
Hata hivyo, inadaiwa kwamba katika vita hiyo Wekundu wa Msimbazi tayari wanaonekana kushindwa baada ya Ajib kutaka apewe Sh milioni 100 ili akubali kusaini kuichezea timu hiyo ambayo juzi imetangazwa kuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara.
Inaelezwa kuwa viongozi wa Yanga kwa kushirikiana na matajiri wengine wa timu hiyo, tayari wameanza mazungumzo na nyota huyo kwa ajili ya kumpa mkataba mpya




0 Comments