

NA ZAITUNI KIBWANA
SIMBA sasa mambo ni motooo, kila kitu balaa baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’, kutema cheche Dar es Salaam jana kwa kutangaza mikakati kabambe, ikiwamo kambi watakayoweka nchini Ureno anakotoka nyota anayekipiga Juventus ya Italia, Cristiano Ronaldo au Marekani.
Mpango huo ni moja ya mikakati yao ya kuhakikisha wanajipanga vema tayari kukinukisha msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini pia katika michuano ya kimataifa wakitarajia kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi za MeTL Group zilizopo jengo la Golden Jubilee Towers, jijini, Mo Dewji alisema Bodi ya Wakurugenzi imepania kuifanya timu hiyo kuwa tishio zaidi msimu ujao.
Kambi kwa Ronaldo au Rooney
Mo alisema wanatarajia kikosi chao kuweka kambi Ureno au Marekani anakocheza straika wa zamani wa timu ya Taifa ya England, Everton na Machester United, Wayne Rooney anayechezea D.C United kujiandaa na msimu ujao.
“Mimi binafsi naongea na klabu za Ulaya, nina rafiki yangu mmoja bahati nzuri anamiliki timu ya D.C United, timu wanayocheza akina Rooney na nimeongea naye nimeomba watualike kwa ajili ya maandalizi na angalau tucheze na timu yake na tupate mechi nyingine.
“Mwaka jana tulikwenda Uturuki, halafu mwaka juzi Afrika Kusini, kwa hiyo mwaka huu tutaona kama kuna uwezekano wa kwenda Ureno ambapo pia nilikutana na viongozi wao, kule kuna timu nyingi za Ligi Kuu asilimia 70 zinatoka Kaskazini mwa Ureno, hilo pia tunafikiria.
Alisema Mungu akijalia, ndani ya wiki mbili zijazo watapata mwanga ni wapi timu yao itaweka kambi kati ya Ureno au Marekani.
Aussems aandaliwa mkataba mnono
Juu ya Kocha Mkuu wao, Patrick Aussems, bilionea huyo alisema wanatarajia kumwongezea mkataba mpya ili aendelee kukinoa kikosi chao baada ya msimu huu kuwapa mafanikio makubwa, akiwafikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini pia wakitetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara.
“Bodi ya Wakurugenzi tumeshaamua kocha (Aussems) amefikisha malengo, tulikuwa tunataka ubingwa na kufika makundi Ligi ya Mabingwa, lakini hiyo pia alivuka na kufika robo fainali, Mungu akitujalia kwenye wiki moja tutakaa naye ili tuweze kumwongezea mkataba tuendelee naye.
“Aussems tayari anafahamu mazingira ya nchi yetu, anafahamu wachezaji wetu, anajua falsafa ya Simba, anajua utamaduni wetu… kwahiyo tungependa sana aendelee na Bodi ya Wakurugenzi wameshakubali kumwongezea mkataba na tutamweleza wapi kuna mapungufu,” alisema Mo.
Bilionea huyo kijana zaidi Afrika, alisema moja ya mapendekezo ya Aussems ni kuongezewa tabibu kwenye benchi la ufundi mwenye uwezo wa hali ya juu katika kutibu majeraha ya wachezaji na kuwa karibu nao.
Wataka ‘mwali’ wao Jumamosi
Mo Dewji alisema wapo kwenye mawasiliano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ili ikiwezekana katika mechi yao na Biashara United itakayopigwa Jumamosi hii, wakabidhiwe Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
“Tunaomba sana mashabiki wajitokeze kwa wingi kwenye hiyo mechi ambayo tutakabidhiwa kikombe chetu cha ubingwa,” alisema.
Mo aliwataka mashabiki wao kuendelea kupiga kura za tuzo maalumu zilizoandaliwa kwa ajili ya wachezaji wao bora wa msimu huu.
“Mei 30 tutakuwa na Mo Awards, tunaomba sana wana Simba wajitokeze na waendelee kupiga kura kwa wachezaji ambao wao wanawapenda ili kuendelea kuleta hamasa,” alisema.
Vipi kuhusu mechi yao na Sevilla leo?
Mo alisema hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kucheza na timu inayoshiriki michuano ya La Liga na kuwataka mashabiki wajaze uwanja kama walivyokuwa wanafanya kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.
“Ni historia kwa ajili ya Simba, tunawashukuru SportPesa kwa kuwaleta nchini, tumejipanga kucheza na Sevilla kama Simba,” alisema.
Usajili
“Simba tupo makini sana kwenye suala la usajili, tunatarajia kupokea ripoti ya kocha ya wachezaji anaowataka kwa ajili ya kuongezea mikataba.
“Simba itafanya juu chini kuwaongezea mikataba wachezaji ambao watapendekezwa lakini pia kati ya wachezaji 10 wa kimataifa, pia itajulikana ni yupi kocha amemtaka aendelee kusajili kwenye kikosi chetu na wale ambao wataachwa watajulikana.
“Simba itakuwa kwenye soko la kushindana na Al Ahly (Misri), Zamalek (Misri) na TP Mazembe (DR Congo) kupata wachezaji kwenye Bara la Afrika, kuna wale watakaotolewa kwa mkopo na wageni ambao tutafanya juu chini kuweza kuwanunua na kuwaleta,” alisema.
Alipoulizwa bajeti waliyotenga kwa msimu ujao, Mo aligoma kutaja na kusema: “Bajeti rasmi bado hatujaipitisha kwenye bodi ya wakurugenzi, lakini itakuwa kubwa kuliko bajeti ya mwaka jana,” alisema.
Awapa ‘boxer’ wachezaji wote Simba
Mo amewapa wachezaji wa Simba bodaboda aina ya ‘boxer’ kama zawadi baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.
“Nilifanya kikao na wachezaji kama kutoa hamasa, nimeahidi nitawapa wachezaji wote pikipiki ya ‘boxer’ ambayo inauzwa kwa Sh milioni 2.4.
“Nimewaambia wawekeze hiyo pikipiki kwa kumtafuta ndugu ambaye ataweza kumletea Sh 15,000 kila siku kwenye mwaka mzima hiyo pikipiki moja inaweza kuzaa Sh milioni 5 na baadaye hiyo pikipiki anaweza kumwachia yule ndugu yake ili na yeye aendeshe maisha yake,” alisema.
Aipa tano Yanga
Mo amewapongeza Yanga kwa kuonyesha ushindani msimu huu licha ya watani wao hao kuukosa ubingwa uliotua Msimbazi.
“Nawapongeza Yanga kwa hatua waliyofikia, wameleta changamoto kubwa, nawashauri wajipange upya kwa msimu ujao kwani ushindani utakuwa mkubwa, lakini pia nawapongeza viongozi wao wapya waliochaguliwa,” alisema.
Bilioni 20/- bado hazijatoka
Mo amesema bado hajatoa Sh bilioni 20 alizoahidi kwa ajili ya kununua hisa za asilimia 51 za kuwekeza ndani ya klabu hiyo.
“Tulikubaliana na Simba nitachukua mali na madeni, lakini kukawa na tatizo la kuhifadhi mapato yao vizuri, tukashindwa kwa sababu kulikuwa hakuna mahesabu.
“Kuhamisha mali na madeni lazima mahesabu yakamilike na si ya mwaka mmoja ni ya miaka mitatu ila sasa tayari fedha nimeikabidhi kimaandishi lakini rasmi haijaingia tunangojea makubaliano ya mali ihamishwe na pesa iingie,” alisema.




0 Comments