

KWA mujibu wa madaktari, kifo cha mwanamuziki Golden Jacob Mbunda ‘Godzilla’ kilitokana na mchanganyiko wa malaria, kupanda kwa kisukari na kushuka kwa presha.
Dada wa marehemu Godzilla aitwaye, Joyce Mbunda, amesema hivyo katika mahojiano aliyofanya na Global TV Online ambapo amesema matatizo yaliyopelekea kifo cha mwanamuziki huyo kijana yalianza Jumapili iliyopita alipokuwa anajisikia vibaya hali iliyosababisha wampeleke hospitali.
Joyce amesema baada ya kumfikisha hospitali na kupimwa, daktari alisema tatizo lilikuwa ni malaria, kupanda kwa kisukari na kushuka kwa presha, hivyo alimpa dawa za kukabiliana na tatizo hilo na wakaruhusiwa kurudi nyumbani.
Hata hivyo, baada ya kurudi nyumbani, marehemu alizidi kutapika akidai kulikuwa kuna kitu kimemkwama tumboni na kwamba nguvu zilikuwa zinamwishia, hali ambayo iliwalazimu kumrudisha hospitali tena kwa ajili ya matibabu alikoendelea kupata matibabu hadi jana waliporudi nyumbani.
Akiwa nyumbani akiendelea kupata dawa chini ya uangalizi wao, aliingia chumbani kulala lakini, kwa mujibu wa Joyce, kaka yake alianza kusema aliona watu wanamfuata na hivyo kumwomba amfiche wasimfuate ambapo ilibidi wamshike asizidi kuhangaika.
Ni wakati wakiwa wamemshika ndipo Godzilla mmoja wa wanamuziki maarufu nchini katika midundo ya Bongo Fleva alikata roho usiku wa kuamkia leo na kufariki dunia.




0 Comments