

KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema milango iko wazi kwa beki wao, Salimu Mbonde ambaye hakuwa na msimu mzuri Msimbazikutokana kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha.Mbonde tangu asajiliwe Msimbazi akitokea Mtibwa Sugar misimu miwili iliyopita amecheza mechi chache ikiwamo moja ya msimu uliopita kutokana na majeraha.
Mechi ya mwisho ya Mbonde aliyocheza Simba ilikuwa dhidi ya Kagera Sugar, wakati wakikabidhiwa ndoo ya ubingwa msimu uliopita na Rais John Magufuli kabla ya kutoka akiwa hajatumia hata dakika 10 tena akilia kutokana na kujiumiza tena.
Baadaye Simba ilimpeleka Mbonde kutibiwa Afrika Kusini, lakini tangu msimu huu uanze hajaonekana katika mazoezi ya pamoja na timu na sasa unaelekea ukingoni.
Katwila alisema anaimani na kipaji cha mchezaji huyo na endapo itabainika amepona na timu yake ya mwisho kuichezea ikashindwa kumuongeza mkataba, basi atafanya mpango wa kumuita kikosini kwake.
“Mbonde amelelewa na Mtibwa ni zao letu, hivyo kama hali yake imetengamaa na yeye ameridhia kujiunga na timu yake ya zamani milango iko wazi tutamrudisha kwasababu mpira ndio maisha yake tutakaa mezani tukiyamaliza ataonekana tena uwanjani msimu ujao,” alisema Katwila.
“Ni mapema sana kuzungumzia nafasi zinazotakiwa kusajiliwa muda huu ligi ikiwa bado haijaisha namzungumzia Mbonde kwani hayupo kwangu, ila ni mchezaji ninayetambua uwezo wake, tusubiri kuona ni timu gani inaweza kumpa mkataba.”



0 Comments