


KAMA unadhani Yanga wanauonea donge ubingwa wa Simba, utachemka baadhi ya nyota wa Yanga, walisema Simba walistahili taji kwani walipambana, ila wanajipanga kwa msimu ujao.
Viungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Deus Kaseke, waliipongeza Simba kwa mafanikio hayo akidai wanastahili kutokana na juhudi waliyoionyesha wakati wanacheza mechi zao za viporo.
“Hakuna kitu kigumu kama mpinzani wako anaongoza ligi kwa muda mrefu na kama mchezaji ni mwepesi wa kukata tamaa unaweza kuvunjika moyo, nimejifunza kitu kwa mastaa wa Simba ambao hawakujali badala yake waliendelea kujituma,” alisema.
“Ninachokizungumza anayeweza kunielewa kisawasawa ni mchezaji ama mtu wa soka kindakindaki, Simba wanastahili pongezi kwani wamefanikisha hilo dakika za jioni haikuwa rahisi kwao kupata mafanikio hayo.
“Kwanza wamecheza mechi nyingi kwa maana ya Ligi ya Mabingwa Afrika na msimu huu mzunguko ulikuwa mkubwa lakini walicheza Kombe la FA licha ya kutolewa mapema najua ni kiasi gani wachezaji wa Simba watakuwa wamechoka kwa kutumika sana, nawapongeza na sisi tunajipanga kwa msimu ujao,” alisema.
Naye Kaseke amewapongeza wachezaji wa Simba kwa kazi ngumu waliyoifanya katika msimu huu.



0 Comments