Windows

Dau la mazembe kwa Ajibu


WAKATI straika Heritier Makambo akitupia bao lake la 17 katika Ligi Kuu Bara, huku akiaga kabla ya kutimka zake Ubelgiji, dau la kumng’oa fundi wa mpira, Ibrahim Ajibu anayetakiwa na TP Mazembe limeanikwa, huku akiwa na mkataba wa awali wa Simba.


Ajibu, anayeongoza kwa kuasisti katika ligi ya msimu huu akitoa pasi 15 za mabao huku mwenyewe akifunga sita, yupo mbioni kujiunga na Mazembe ambayo imetuma barua Yanga ili kumbeba mara baada ya mkabata wake kumalizika Juni 30 mwaka huu.


Mazembe imewaandikia barua Yanga kuwajulisha kuwa watamchukua Ajibu rasmi Julai mosi 2019 na kwamba kama kuna utofauti wowote wa taarifa hiyo Yanga iwasiliane nao kwa mujibu wa Kanuni za Usajili za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).


Habari za kuaminika kutoka Yanga zinasema, Mazembe wapo tayari kumbeba Ajibu kwa kitita cha zaidi ya Dola 25,000 (karibu Sh 60 Milioni), mbali na mshahara mnono na huduma nyingine zikiwamo usafiri, makazi na posho nyingine za kutosha.


Chanzo hicho kilidokeza mkataba wa nyota huyo umetazamwa katika vipengele muhimu ikiwa sambamba na fedha ya mshahara na nafasi ya kumruhusu kutoka endapo atapata timu nyingine ya kucheza.


“Unajua kitu kikubwa ambacho wamekiangalia viongozi wanaomsimamia ni dau la mshahara wake kwa mwezi na nafasi ya kumuachia akipata timu yoyote nje ya nchi, lakini sijafahamu atakuwa anapata kiasi gani, ila nasikia ni fedha nzuri ndio maana wameamua kumpeleka,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;“Pia naweza kusema ni muda wa Ajibu kwenda kujaribu soka la kulipwa nje ulikuwa umewadia kwani bado alikuwa na nafasi ya kucheza Tanzania kwani, Yanga na Simba zote zilikuwa zinahitaji huduma yake, ila wameshindwa kuweka fedha aliyokuwa anaitaka mezani,” kilisema chanzo hicho kilidokeza.


Katika dili hilo Yanga ni wazi haitapata fedha zozote kwani usajili huo umekuja Ajibu akiwa amemaliza mkataba, huku ikielezwa Simba walishamsainisha mkataba wa awali wa kumsajili kabla ya Moise Katumbi na watendaji wake kutaka kupindua meza.


MAKAMBO ATUPIA AKIAGA


Akiwa anajiandaa kuondoka Jangwani, Heritier Makambo jana Jumatano jioni alifunga bao pekee likiwa la 17 kwake katika Ligi Kuu wakati Yanga ikiizamisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam katika mchezo uliohudhuriwa na mashabiki wachache.


Makambo alifunga bao hilo katika dakika ya 26 kwa kichwa na kuipa Yanga ushindi wa 27 msimu huu na kukusanya alama 86 na mabao 56 ya kufunga, ingawa hayana faida kwani, Simba tayari imeshanyakua ubingwa baada ya juzi Jumanne kuifumua Singida United mabao 2-0.


Mara baada ya kufunga bao hilo Straika huyo, alionyesha ishara yake ya ‘kuwajaza’ kisha akaziba masikio na kuonyesha ishara ya kuomba radhi kama akiwaangukia mashabiki wa Yanga na sasa anajiandaa kuondoka kwenda Ubelgiji kujiunga na klabu ya Waasland Baveren ambaye Wakala wake Raoul Alfred alitinga uwanjani kumshuhudia Makambo.


Mwakilishi wa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji (Pro Jupiler) alitinga uwanjani kipindi cha pili akiambatana na viongozi wa Yanga na kwenda jukwaani kumshuhudia Makambo akiupiga sambamba nyota wenzake walioifunika Mbeya City.


Katika mechi hiyo, Yanga iliwabana City waliotoka kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Lipuli, licha ya kuwakosa nyota saba akiwamo Ajibu walio na matatizo mbalimbali.


Mara baada ya mchezo huo, makambo alisema anaondoka Yanga lakini akiikumbuka kwa mengi huku akimtaja Kocha Mwinyi Zahera, Afisa Habari Msaidizi wa Yanga, Godlisten Chicharito na mashabiki wa klabu sambamba na wachezaji wenzake alioshirikiana nao.


Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Mwadui ilizinduka kwa kuikamua African Lyon mjini Mwadui, Shinyanga kwa mabao 3-0, huku Salim Aiyee akifunga bao la tatu na kufanya kula sahani moja na Makambo akifika mabao 17, huku Lipuli ikilazimisha sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Ndanda.


Post a Comment

0 Comments