KLAUS Kindoki, mlinda mlango wa Yanga, licha ya kuibuka shujaa kwenye mchezo wa juzi wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) kwa kuipeleka timu yake nusu fainali baada ya kuokoa penalti mbili, amemuachia neema mshambuliaji wa Alliance FC, Joseph James.
James alifanikiwa kumfunga Kindoki dakika ya 62 kwa bao la kichwa, hali iliyofanya mchezo huo wa Kombe la Shirikisho uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ufikie hatua ya matuta baada ya sare ya 1-1 na Yanga kushinda 4-3.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Ofisa Habari wa Alliance, Jackson Mwafulango, alisema kuwa mfungaji wa bao atapewa shilingi milioni moja ila wanaumia kupoteza mchezo wao wa robo fainali licha ya kupambana mpaka kufika hatua ya penalti.
“Tuliwaahidi wachezaji wetu kwamba wakishinda tunawapa fedha ili kuongeza morali na kupambana kwao uwanjani, sasa James ndiye amefanikiwa kufunga bao, huyo lazima apewe fedha yake ambayo ni milioni moja na wachezaji wetu wote nao pia huwa tunawapa fedha endapo wakishinda mchezo, lengo letu ni kuondoa yale matabaka endapo tutasema tunampa mchezaji mmoja,” alisema Mwafulango.
0 Comments