KOCHA wa Azam FC, Meja Abdul Mingange amesema kuwa uzoefu umewaponza wachezaji wake hali iliyowafanya wakafungwa bao 1-0 na Yanga kwenye mchezo wao wa ligi uliochezwa jana uwanja wa Uhuru.
Azam FC ilifungwa bao hilo na Mrisho Ngasa ambaye alikuwa mchezaji wao wa zamani dakika ya 13 na lilidumu mpaka mwisho wa mchezo na kuwafanya wapoteze pointi tatu muhimu.
Akizungumza na Saleh Jembe, Mingange amesema kuwa walijipanga kiasi cha kutosha kupata ushindi kwenye mchezo wao ila walizidiwa uzoefu na wapinzani wao ambao walidhamiria kushinda.
"Haikuwa mipango yetu kupoteza mchezo wetu mbele ya Yanga, tulijipanga kiasi cha kutosha kushinda ila uzoefu wa wachezaji wangu ukatufelisha kwenye mchezo wetu.
"Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wengi ambao wanauzoefu na ligi tofauti na sisi, licha ya kutengeneza nafasi nyingi kwenye mchezo wetu tulishindwa kupata matokeo kutokana na kushindwa kuzitumia nafasi tulizotengeneza," amesema Mingange.
Azam FC wanasalia nafasi ya tatu wakiwa na pointi 66 baada ya kucheza michezo 33 kwenye ligi kuu huku Yanga wakijikita kileleni na pointi zao 77 kibindoni.
0 Comments