Ulikuwa usiku wa fedheha kubwa katika uwanja wa Santiago Bernabeu. KWA MARA NYINGINE TENA. Lakini mara hii, sio kutoka kwa mahasimu wao wa La Liga Barcelona. Ni kutoka kwa chipukizi wa Amsterdam, Ajax. Mabingwa hao watatezi Real Madrid ambao kabla msimu huu walikuwa wamelibeba taji hilo mara tatu mfululizo, wameondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho na Ajax Amsterdam ya Uholanzi. Madrid walishindiliwa magoli 4-1 mbele ya mashabiki wao wa nyumbani na kuondolewa kwa jumla ya magoli 5-3 baada ya kutoa ushindi wa 2-1 katika mechi ya duru ya kwanza. Ni mechi ambayo vijana wa Ajax waliidhibiti katika kipindi kirefu na wangeweza hata kufunga mabao mengi zaidi.
Kwingineko, vinara wa ligi kuu ya Ujerumani – Bundesliga Borussia Dortmund wamebanduliwa katika hatua ya 16 za mwisho baada ya kulazwa bao moja kwa bila na Tottenham Hotspur nyumbani kwao Signal Iduna Park. Mshambuliaji wa Spurs Harry Kane ndiye aliyefunga goli la pekee la mechi hiyo katika dakika ya arubaini na nane ya mechi. BVB wameyaaga mashindano hayo kwa kuduwazwa jumla ya mabao 4-0 baada ya kufungwa 3-0 Uingereza katika mechi ya mkumbo wa kwanza.
0 Comments