UONGOZI wa Simba umepeleka maombi maalum kwa Bodi ya Ligi inayofanya kazi kwa karibu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuomba mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania kupangiwa tarehe nyingine.
Simba itatakiwa kucheza dhidi ya wapinzani wao hao katika mechi ya Ligi Kuu Bara mnamo Aprili 3, mwaka huu, kisha Aprili 6 inatarajiwa kuwa na kibarua mbele ya TP Mazembe katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Hatua ya Robo Fainali.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema kwa sasa wanasubiri majibu tu ambayo watayapata kutoka TFF baada ya kupeleka maombi yao.
“Tumepeleka maombi yetu kwa TFF kuona namna gani tunaweza kufanya ili tupate muda wa kujiandaa kwa mechi yetu ya kimataifa dhidi ya Mazembe, tunataka mechi dhidi ya JKT Tanzania isogezwe mbele.
“Barua ilishakwenda, kwa hiyo sasa hivi tunasubiri majibu yao tuone yako vipi wakati tukiendelea kujiandaa na mechi yetu na Mbao FC,” alisema Rweyemamu.
0 Comments