

HAKIMU Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar, Kelvin Mhina, amesema upande wa serikali unatakiwa kuiambia mahakama imefikia hatua gani katika upelelezi wa kesi inayomkabili aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura.
Hakimu huyo alisema serikali inatakiwa kueleza katika upelelezi wao wamefikia hatua ipi ili upande wa pili waweze kufahamu.
Wambura anakabiliwa na mashitaka yapatayo 17 likiwemo la utakatishaji fedha na kughushi nyaraka ambayo hayana dhamana.
Wakili wa serikali, Elizabeth Nkunde, aliiambia mahakama kuwa hadi sasa bado upelelezi haujakamilika na anaomba ipangwe tarehe nyingine ya kesi kusikilizwa.
Aidha, wakili wa mshitakiwa, Nestory Wandiba aliyemwakilisha Majura Magafu, aliiambia mahakama kuwa serikali, inatakiwa kuhakikisha upelelezi unakamilika mapema ili mshitakiwa atendewe haki.
Kutokana na upelelezi kushindwa kukamilika, kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 11, mwaka huu na mshitakiwa anaendelea kusota rumande kama ilivyo kawaida ya kesi za utakatishaji fedha.




0 Comments