Windows

AS Vita: Tunakuja Dar Yanga tupokeeni




KOCHA wa AS Vita ya DR Congo, Raoul Shungu, amesema kwamba hana presha na Simba kuelekea mchezo baina yao wa Jumamosi hii kwani hata kama watafanya fitina za aina gani, Wekundu wa Msimbazi hawataambulia lolote kwani anafahamu njia zote za kupitia kukwepa vigingi vya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ni kutokana na kujiamini kwake huko, Shungu amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kuwapokea Alhamisi hii watakapotua Dar es Salaam akiahidi kuwafurahisha Jumamosi watakapovaana na Simba.


Shungu aliwahi kuinoa Yanga kwa mafanikio makubwa ya kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati nchini Uganda, Kombe la Nyerere mwaka 1999 na Kombe la Muungano mwaka 2000.

Akizungumza nasi kutoka DR Congo jana, Shungu alisema anayafahamu vema mazingira ya soka la Tanzania, hivyo amejipanga vilivyo kuifunga Simba katika uwanja wao wa nyumbani.

“Sina hofu kwa vile tutakuwa ugenini, Tanzania ni nyumbani kwangu pia nimekaa kwa muda wa miaka mitatu, natambua vizuri mazingira yake ya soka, mimi nimejiandaa vyema kama mwalimu kwa uzoefu wangu, nina uhakika tutapata ushindi,” alisema Shungu.

Shungu alisema kuwa tayari timu yake imeshajiandaa kwa ajili ya mchezo huo na wanatarajia kutua nchini Alhamisi hivyo kuwataka mashabiki wa Yanga kuwapa sapoti.

Kocha huyo alisema wachezaji wake wapo fiti kwa asilimia 100, akiwa hana majeruhi yeyote, akijiandaa kutua nchini na wachezaji 20 tayari kuwapa Simba kipigo kingine cha nguvu baada ya kile cha mabao 5-0 walichowapa nchini kwao.

“Nitakuja na wachezaji wangu wote watatu wa kimataifa walioitwa kwenye timu zao za taifa kwa ajili ya maandalizi ya fainali za Kombe la Mataifa Afrika na nitawaruhusu kuungana na timu zao za taifa baada ya kucheza na Simba kwani ni wachezaji muhimu mno kwetu,” alisisitiza.

Shungu aliwataja wachezaji hao kuwa ni Savio Kabugo wa Uganda, Oumar Sidibe wa Senegal na Akwo Ayuk wa Nigeria.

Post a Comment

0 Comments