Baada ya hivi karibuni, Yanga kushindwa kufanya vizuri katika michuano ya SportPesa iliyofikia tamati jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kocha mkuu wa timu hiyo raia wa DR Congo, Mwinyi Zahera anajipanga kuhakikisha msimu ujao anachukua nafasi ya Simba kwenye michuano ya kimataifa inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Katika kufanikisha hilo, Zahera ameandaa mikakati kabambe kwa Yanga ambayo ni kuhakikisha timu hiyo kuanzia sasa haipotezi mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara kati ya 18 ilizobakiza.
Hivi sasa Yanga inaongoza msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 53, ilizojipatia baada ya kucheza mechi 20 huku ikishinda 17, ikitoka sare mara mbili na kufungwa mmoja.
Zahera alisema kuwa endapo lengo hilo litatimia, mikakati yake ya kuiona Simba haishiriki michuano yoyote ile ya kimataifa inayosimamiwa na Caf msimu ujao, itakuwa imetimia kama wao ambavyo msimu huu hawakushiriki michuano yoyote inayosimamiwa na shirikisho hilo.
“Hilo ndilo lengo langu kubwa kwa sasa na hakuna kitu kingine ambacho ninakifikiria katika akili yangu, zaidi ya ubingwa wa ligi kuu pamoja na ule wa Kombe la FA.
“Tunatakiwa kufanya vizuri katika mechi zetu zote 18 za ligi kuu zilizobaki lakini pia zile za Kombe la FA.
“Kwa hiyo nimejipanga kwa hilo na ninaamini kabisa hakuna kitakachoshindikana, kama tuliweza kucheza mechi 19 za ligi kuu bila ya kupoteza katika mzunguko wa kwanza, pia tunaweza kufanya hivyo katika mzunguko wa pili,” alisema Zahera na kuongeza:
“Niwaombe tu wapenzi pamoja na mashabiki wa timu yetu kuendelea kutuunga mkono kama ambavyo wamekuwa wakifanya siku zote ili ndoto yetu hiyo ya kufanya vizuri katika michuano hiyo iweze kutimia.”
0 Comments