Windows

SIMBA WAFUNGUKA HATIMA YAO NA AUSSEMS


Wale mashabiki wa Simba ambao wanataka kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems atimuliwe kutokana na matokeo mabaya ambayo imeyapata hivi karibuni, hii itakuwa ni habari mbaya kwao.

Uongozi wa timu hiyo umesema kuwa hauna mpango wa kuachana na Aussems kwa sasa kwani hauoni sababu ya kufanya hivyo, na kwamba bado wanaridhishwa na utendaji wake wa kazi.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, ameliambia Championi Jumatatu kuwa matokeo mabaya ambayo timu hiyo imeyapata hivi karibuni katika michuano ya SportPesa, yasichukuliwe kama chanzo cha udhaifu wa kocha huyo.

Alisema wakati Aussems anajiunga na Simba, uongozi wa timu hiyo ulikubaliana naye mambo makuu mawili ambayo alitakiwa kuifanyia timu hiyo msimu huu.

Mambo hayo ni kuhakikisha Simba inatetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara lakini pia kuiwezesha timu hiyo kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo ambalo tayari ameshalifanya.

“Alichobakiza ni ubingwa wa ligi kuu tu, kwa hiyo bado uongozi una imani naye na hauna mpango wa kuachana naye kwa sasa,” alisema Manara.

Awali, mashabiki wa timu hiyo walionekana kumkasirikia Mbelgiji huyo, baada ya timu yao kufungwa na Bandari 2-1 katika nusu fainali ya michuano ya SportPesa juzi Ijumaa.

Post a Comment

0 Comments