Mambo ni moto ndani ya Simba! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya uongozi wa timu hiyo kuwachukulia hatua wachezaji wote wanaodaiwa kutoroka kambini na kwenda kufanya starehe wakati wakijua wanakabiliwa na mechi ngumu.
Usiku wa kuamkia Ijumaa, baadhi ya wachezaji wa Simba ambao ni Haruna Niyonzima, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Pascal Wawa, Mohammed Ibrahim ‘Mo’, Mzamiru Yassini pamoja na Hassan Dilunga walidaiwa kutoroka kambini na kwenda kufanya starehe wakati wakijua kesho yake wanakabiliwa na mechi ngumu ya Nusu Fainali ya Michuano ya SportPesa dhidi ya Bandari ya Kenya.
Kutokana na hali hiyo, wachezaji hao kila mmoja amelimwa barua ya onyo ikiwaonya kutorudia kufanya kosa kama hilo siku nyingine.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa, uongozi wa timu hiyo ulitaka kuwakata mshahara wa mwezi mmoja wachezaji hao kutokana na kosa hilo, lakini kocha aliwatetea kwa kuutaka uongozi huo kuwaandikia barua za onyo.
“Jambo hilo liliwakasirisha wengi na uongozi ulikuwa umeamua kuwakata kila mmoja mshahara wa mwezi mzima lakini kocha aliwatetea na kuutaka uongozi uwaandikie barua ya onyo.
“Alifanya hivyo, kwa sababu ndiyo mara yao ya kwanza hivyo siyo vizuri kuwachukulia hatua kali kama hizo jambo ambalo uongozi ulikubaliana nalo na kuamua kuwaandikia barua ya onyo kila mmoja,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Mratibu wa Simba, Abassi Ally hakuwa tayari kusema chochote ila kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems alisema kuwa ni kweli wachezaji hao wamepewa onyo lakini pia amezungumza nao ili kuwakumbusha majukumu yao ya kazi.
0 Comments