Windows

PIENAAR 'MCHEZAJI EVERTON': SIMBA NI MAARUFU KULIKO YANGA - VIDEO


Mmmoja wa wachezaji ambao wamekuwa ni nembo ya Afrika Kusini ni Steven Pienaar ambaye alicheza kwa muda mwingi katika kikosi cha Everton FC kinachoshiriki Ligi Kuu England.

Pienaar kwa sasa amestaafu kucheza soka lakini aliichezea Everton tokea mwaka 2007/2008 akiwa kwa mkopo akitokea Borussia Dortmund. Baadaye 2008, Everton walimnunua akakipiga hadi 2011 alipohamia Tottenham kwa msimu mmoja wa 2011/12 na akarejea Everton kwa mkopo na 2012 hadi 2016.

Akabaki hadi alipoondoka kwenda Sunderland alipocheza msimu mmoja wa 2016/17 kabla ya kurudi kwa Afrika Kusini alipojiunga na Bidvest Wits inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini.

Pienaar yuko nchini kwa ajili ya michuano ya SportPesa Super Cup kwa kuwa ni balozi wa Everton ambaye hushiriki katika Kit for Afrika inayosaidia vijana wasiojiweza kuamini na kuendeleza vipaji vyao. Kiungo huyo aliyeifungia Everton jumla ya mabao 18 katika muda wake wote, amefanya mahojiano mafupi maalum na Championi.

“Kweli pale Everton maisha yalikuwa mazuri sana, ilikuwa ni kama nyumbani na wakati mwingine unajiona ni sehemu ya maisha ya pale.

“Ukianza na viongozi, wachezaji wenyewe lakini mashabiki wanakufanya uone kuna watu nyuma yako na wanataka kufanya vizuri.

“Everton ni sehemu ambayo utatamani kuendelea kuwa pale na kufanya vizuri zaidi na zaidi,” anasema.

Kuhusiana na suala la yeye kuondoka na kwenda Tottenham lakini baadaye akarejea tena Everton.

“Ni kweli, maisha ya wanasoka yana hatua, kawaida unatamani kupiga hatua zaidi. Nilitaka kujifunza zaidi, angalia kama vile kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini baadaye nilirejea nyumbani tena (Everton),” anasema.

Championi liliona limrejeshe nyumbani Afrika Kusini na kumuuliza namna Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) kwamba ina maendeleo kwa maana ya vifaa na wadhamini wa kutosha lakini hakuna maendeleo ambayo wengi wangeyatarajia na hivyo kuzifanya nchi za Magharibiki au Kaskazini kuendelea kufanya vizuri zaidi katika Bara la Afrika na kuendeleza utawala.

“Ni kweli, wachezaji wengi wa Afrika Kusini hawapendi kutoka nje ya nchi. Mfano kama wakisikia unakwenda kucheza Cameroon au Congo. Mara nyingine wanakwenda tu kwa kuwa wanatakiwa kufanya hivyo, la sivyo wasingeenda kabisa.

“Hili ni moja ya tatizo na ni kubwa, kama tutabadilika litatusaidia sana. Hakuna ubishi hauwezi kuwa bora bila ya kupambana na wale wanaoaminika ndiyo bora.

“Hivyo lazima wachezaji wabadilike na kukubali kupambana Afrika kwa ajili ya kuonyesha ubora wao, jambo ambalo linawezekana,” anasisitiza.

Kuhusiana Simba na Yanga, timu ambazo ni kubwa hapa nyumbani pia Afrika Mashariki. Hakuna iliyoingia fainali ya SportPesa Super Cup. Gazeti lilitaka kujua kama anajua lolote kuhusiana na mpira wa Tanzania au klabu hizo kongwe.

“Hapana, najua kiasi sana. Pia hata hizi timu mbili nimezisikia mara kadhaa lakini sijui zaidi. Kikubwa najua Simba ni maarufu zaidi ya Yanga hasa nje ya hapa,” anasema.

Pamoja na hivyo, Pienaar anaamini timu za Tanzania zina nafasi ya kufanya vema barani Afrika, lakini anasisitiza.

“Ni lazima ujue unapokwenda kucheza nje ya hapa, mfano unakutana na timu za Kaskazini, lazima ujiandae hasa.

Steven Pienaar (kulia) akiwa na mhariri na mchambuzi wa Michezo kutoka Gazeti la Championi, Saleh Ally.

Lazima ujue kwamba kuna ugumu na utofauti.

“Kama unafanya vizuri katika kiwango cha michuano ya Afrika maana yake una nafasi ya kufanya vema na kujulikana sana ukiwa unaitangaza nchi yako.”

Mwisho kwa kile ambacho wanakifanya SportPesa kwa ukanda wa Afrika Mashariki, mfano Tanzania na Kenya lakini hadi Afrika Kusini ambako wanadhamini michezo na hasa soka. Lakini pia wamekuwa wakiwadhamini au kuwapa vifaa vijana ambao wana vipaji lakini hawana vifaa au wa kuwanunulia. Wamekuwa wakifanya kupitia programu yao Kit For Afrika.

Je, yeye anaizungumziaje.

“Hili ni jambo jema, unajua watoto hawana vifaa wangependa kujiendeleza. Kit For Afrika inasaidia kuwaendeleza, kuwainua na kuwakumbusha kwamba inawezekana, ni jambo bora na sahihi.

“Kwa udhamini, hakuna mafanikio katika soka au mchezo wowote bila ya wadhamini. SportPesa wanachofanya ni sahihi na wanapaswa kuonyeshwa wanachokifanya ni sahihi kwa kupata thamani ya udhamini wao,” anasema.

Mashuja wa timu nyingi za Ulaya kama ilivyo na Everton hurejea kufundisha, mfano Ole Gunnar Sloskjaer amerejea na sasa anainoa Manchester United. Je, yeye atarejea Everton na kuinoa, au mpango wake ni upi?

“Hapa ni suala la vigezo, kweli una vigezo. Natarajia nitafikia huko na baada ya hapo, inawezekana nikarejea na kufanya hivyo lakini acha tusubiri kwanza.”


Post a Comment

0 Comments