


Simba ilikumbana na kipigo hicho kikubwa cha kwanza kwa miaka ya karibuni katika michuano ya kimataifa dhidi ya wenyeji wao, AS Vita ya DR Congo na kuiporomosha kutoka kileleni mwa msimamo hadi nafasi ya tatu katika Kundi D.
Matokeo hayo ya Simba yamewafanya wadau mbalimbali wa soka hapa nchini kuvunja ukimya na kueleza sababu ilichoiponza timu hiyona kuipa mchongo wa maana ili iendelee kutisha zaidi katika michuano ya CAF.
Wengi wamainyooshea kidole safu ya ulinzi ya timu hiyo iliyokuwa chini ya Pascal Wawa, Juuko Murshid, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Nicholas Gyan, wakidai mabeki hao walifanya makosa mengi yaliyochangia Simba kuaibishwa ugenini bila kutarajiwa na mashabiki wengi.
Mchambuzi wa maarufu wa soka nchini Ally Mayay, alisema Simba ilifungwa kwa kushindwa kuwaheshimu wapinzani wao ambao walikuwa bora kuliko wao ndio maana wakafanya makosa mengi yaliyowagharimu.
Mayay alisema Kocha wa Simba, Patrick Aussems alitakiwa kuwa na mbinu nyingi za kucheza kuelekea katika mechi hiyo, lakini pia mbinu aliyoitumia ilishindwa kufanya vizuri ila hakutaka kubadilisha ndio maana vijana wake waliokota idadi kubwa ya mipira nyavuni mwao.
“Nilitegemea kuiona Simba ikifanya mabadiliko ya kupunguza washambuliaji na kuongeza mchezaji katika safu ya ulinzi, lakini ilikuwa tofauti na hivyo na hata mabadiliko yaliyofanya yalikuwa na madhumuni ya kushambulia, hizi sio mbinu za makocha wa Kizungu,” alisema.
“Wachezaji wa safu ya ulinzi hawakuwa katika viwango bora, kwani mabao waliyofungwa ni kutokana na udhaifu wa kutokukaba mpaka mwisho, ukiondoa mkwaju wa penalti,” alisema.
Mayay alisema hata benchi la ufundi na wachezaji wanatakiwa kuyafanyia kazi makosa yote kabla ya kuwafuata Al Alhy mwanzoni mwa mwezi ujao ili kujiweka pazuri kwani nafasi bado wanayo kundini licha ya kipigo hicho cha aibu.
Naye kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’, alisema wachezaji wote wa Simba walizidiwa uwezo binafsi wa kushindana na wenzao wa AS Vita, lakini pia wenyeji walitengeneza nafasi nyingi za kufunga kuliko wao.
Mwaisabula alisema mabeki wote wa Simba hawakuwa na maelewano mazuri na kusababisha kufungwa mabao ya aina moja ambayo kama wangekuwa vizuri katika mechi hiyo wasingeruhusu mabao kama yale mepesi katika mechi kubwa ya aina ile.
“Wachezaji wa AS Vita walikuwa wanacheza tena kwa kupiga pasi za haraka ambazo walionesha fika walikuwa wanataka ushindi katika mechi ile wakati Simba wao muda mwingi walionekana kuwa na uwezo wa chini kabisa katika kucheza hata kushambulia kwao,” alisema Mwaisabula.
Hata Kipa wa zamani wa Simba, Mohammed Mwameja pamoja na wakali wenzake wa zamani Ulimboka Mwakingwe na Zamoyoni Mogella walisisitiza tatizo lililoiangusha Simba jijini Kinshasa ni mabeki wake kukaba kwa macho badala ya miguu.
Mwameja alisema kuanzia viungo wakabaji na mabeki wote wanne wa Simba walishindwa kufanya kazi yao ya kukaba kwa uhakika mpaka mwisho wapinzani wao ambao walikuwa wakipata nafasi za kufunga tena wakiwa wenye aina ya mabao ambayo yalikuwa yakifanana.
“Simba ilicheza na timu yenye wachezaji wazoefu wa mashindano hayo makubwa na kitendo cha kutokuwa na safu nzuri ya ulinzi ilikuwa lazima ipoteze mechi hiyo tena hata zaidi ya mabao iliyofunga, lakini naimani Kocha Aussems ameliona hilo na huenda katika mechi na Al Alhly anaweza kuboresha, kufanya marekebisho au mabadiliko katika safu ya ulinzi,” alisema Mwameja.
Mogella alienda mbali na kudai aliyesababisha Simba kufungwa ni Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera aliye na ukaribu na Kocha wa AS Vita, hivyo kuuza ramani kwa wapinzani wa Msimbazi.
Mogella alisema ukweli ni kwamba Congo hakuna mtandano lakini kwangu naona ukaribu waliokuwa nao, Zahera na Florent Ibengé utakuwa umewasaidia AS Vita kuwa na taarifa zote muhimu za KUIKABILI Simba.



0 Comments