Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameridhia kutimuliwa kwa mkandarasi wa Kampuni ya Mazongela Building Construction, ambaye alipewa kazi ya kujenga tangi la maji la mradi wa Kijiji cha Boga na Mengwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani baada ya kushindwa kutekeleza mradi huo wenye thamani ya Sh milioni 536.
Aidha ameagiza mkandarasi huyo asipewe kazi tena katika wilaya hiyo kwani ameonesha uwezo wake ni mdogo, hawezi kutekeleza ili kuwaondolea kero wananchi wa vijiji hivyo zaidi ya 5,000.
Aweso ameyasema hayo kwenye Kijiji cha Boga unapojengwa mradi huo wakati wa ziara yake kutembelea miradi mbalimbali ya maji, ili kujua maendeleo yake na changamoto zinayoikabili katika kutekeleza miradi hiyo kwenye Halmashauri ya Kisarawe.
Amesema miradi mingi ya vijijini inachangamoto kubwa mojawapo ni baadhi ya wakandarasi kushindwa kukamilisha miradi kutokana na kushindwa kufanya kazi wanazoomba, baadhi hawana uwezo lakini wanapewa kazi hizo jambo ambalo linasababisha kero ya ukosefu wa maji kuendelea.
Mradi tangu Oktoba mwaka jana hadi jana kachimba shimo tu, huu ni ubabaishaji ambao hautakiwi uendelee hapa, hakuna maneno zaidi ya kuongea inatosha mkandarasi huyu kaumiza watu kwa muda mrefu hatufai tushamwondoa na hakuna lugha nyingine tusiimbe tu kuwa mkandarasi hana uwezo tutafute wale wenye uwezo," amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo alisema inasikitisha kuona kuwa mji huo ulianzishwa sawa na mji wa Nairobi nchini Kenya lakini hauna maji.
Mwegelo alisema ukosefu wa maji umesababisha wilaya hiyo ishindwe kuendelea na baadhi ya wakandarasi hawachukuliwi hatua kama kazi wameshindwa waondolewe, viongozi wajitafakari kwa nini wanapewa kazi lakini hawana uwezo.
0 Comments