UNALIKUMBUKA lile jiwe la waashi lilivyokataliwa na baadae lilivyogeuka kuwa jiwe kuu? Achana na mambo hayo kwanza tuje katika maisha ya kila siku kwani sisi binadamu tunaishi kama jiwe lililokataliwa na waashi.
Katika soka la Bongo pia kuna wachezaji ambao ni kama jiwe la waashi baada ya kuchukuliwa poa katika timu zao na kwenda kuwika katika timu zingine.
Mwanaspoti kwa umakini limeangalia nyota hao jinsi ambavyo wanafanya vizuri msimu huu baada ya kuchukuliwa kawaida walipokuwa katika timu zao huku wengine wakifikia hatua ya kutolewa kwa mkopo.
WAZIR JUNIOR
Mshambuliaji huyu hakuwa na msimu mzuri akiwa na kikosi cha Azam FC baada ya kusumbuliwa na majeraha yaliyomfanya akae nje ya uwanja kwa takriban msimu mmoja.
Msimu uliopita aliomba kutolewa kwa mkopo na alikwenda Biashara Utd, lakini pia hakuwa na msimu mzuri hali iliyofikia Azam kutomuongeza mkataba na kuamua kutafuta maisha mengine.
Msimu huu amejiunga na Mbao FC na tayari ameonyesha cheche zake baada ya kutupia magoli manne mpaka hivi sasa, huku akiibuka kuwa mchezaji bora wa mwezi Novemba katika timu hiyo pamoja na kuchaguliwa mchezaji bora katika Ligi Kuu kwa mwezi huo.
YUSUF MHILU
Yanga walimuona hawezi kupambana. Hilo lilijionyesha msimu uliopita na alipotua Kocha Mwinyi Zahera aliamua kumuondoa kikosini na kutimkia zake Ndanda FC kwa mkopo.
Akiwa Ndanda alionyesha uwezo wake wa kucheza nafasi ya winga wa kulia lakini pia kama mshambuliaji wa kati na kuonyesha kwamba nafasi hizo anazimudu vizuri.
Yusuf alikubali kumalizana na Yanga vizuri na baada ya hapo alijiunga na Kagera Sugar msimu huu ambapo amekuwa mchezaji tegemeo katika kikosi hicho huku akifunga magoli manne mpaka hivi kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Mecky Maxime.
BENO KAKOLANYA
Kudai masilahi yake kulimfanya aonekane kama hayupo sawa katika kikosi cha Yanga, mashabiki wa Jangwani wakamkataa pamoja na uongozi.
Simba wamemsajili, lakini ukweli ni kwamba mashabiki wa Simba wana imani naye baada ya kusajiliwa kwani Kakolanya amekuwa na uwezo mzuri tangu akiwa na Prisons.
Akiwa na Simba, Kakolanya ameweza kufanya vizuri katika michezo kadhaa ukiwemo ule wa Ud Songo uliomalizika 0-0 (Msumbiji) na dhidi ya Arusha F walioshinda 6-0 (FA).
PATO NGONYANI
Bila shaka mtu pekee ambaye kiungo huyu hatamsahau ni kocha Hans Pulijm wakati anaifundisha Yanga. Pato alipewa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza mpaka kwenye mechi za timu ya Taifa.
Mabadiliko ya kocha yalimfanya Pato akose namba katika kikosi cha kwanza na kujikuta akitolewa kwa mkopo katika msimu uliopita kwenda African Lyon.
Nyota huyo alifanya vizuri akiwa na Lyon na hata mkataba wake na Yanga ulipomalizika ilikuwa rahisi kupata timu na moja kwa moja, akisajiliwa na Polisi Tanzania msimu huu.
Msimu huu amegeuka kuwa nyota tegemeo baada ya uwezo wake wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji na beki wa kati kuisaidia timu hiyo vilivyo.
PIUS BUSWITA
Kiungo huyu baada ya kumalizana na Yanga alijikuta akikaa mtaani akikosa timu. Wengi waliamini kwamba mchezaji huyo tayari ameshafeli kabisa katika soka.
Uongozi wa Polisi Tanzania wameamua kumrejesha uwanjani baada ya kumsajili kwa mkataba wa miezi sita kwa ajili ya kuisadia timu yao katika Ligi Kuu.
Buswita alitamba akiwa na Yanga lakini ghafla alipotea baada ya mkataba wake kumalizika huku kukiwa hakuna timu iliyoonyesha kuhitaji huduma yake.
DITRAM NCHIMBI
Straika huyu alikuwa hahitajiki katika kikosi cha Azam FC na aliyekuwa kocha wa timu hiyo msimu huu, Etienne Ndayiragije alitamka wazi kwamba hamhitaji mshambuliaji huyu.
Nchimbi hakusita kwani aliondoka na kwenda Polisi Tanzania kucheza kwa mkopo.
Akiwa katika klabu hiyo ameifungia magoli manne huku akikumbukwa kwa kuweza kuivusha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ dhidi ya Sudan baada ya kufunga goli nchini Sudan kuwania kufuzu kwa ajili ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan). Kwa sasa amesajiliwa na Yanga kupitia dirisha dogo, ambapo anakumbukwa kwamba aliwapiga bao tatu Yanga katika mechi ya Ligi Kuu wakati akikipiga Polisi Tanzania na hivyo kuamsha ari ya kumtaka.
0 Comments