Windows

Mbelgiji Sven amrudisha Chama upya ndani ya Simba SC






Katika mchezo wa pili ambao ulikuwa dhidi ya Lipuli katika Ligi, Chama aliendelea kutesa katika mfumo wa 4-5-1 kwa kucheza na Sharaf Shiboub katika eneo la kiungo la juu huku chini akicheza Jonas Mkude katika maeneo ya pembeni walicheza Kahata na Dilunga

ACHANA na mechi ya jana ya Simba dhidi ya KMC, lakini kama umekitazama vizuri kikosi cha Simba ya Sven Ludwig Vandenbroeck katika michezo miwili iliyopita, utakuwa umebaini namna ambavyo Mzambia, Clatous Chama ameanza kutumika tofauti na vile ambavyo alikuwa akicheza chini Patrick Aussems.

Aussems ambaye alikuwa akipenda kutumia mfumo wa 4-4-2, 4-2-3-1, 4-3-3 au 4-5-1, alikuwa akimtumia kiungo huyo mbunifu kama winga wa kushoto au kulia ambaye alikuwa akiibia ndani katika eneo la kati licha ya muda mwingine pia kucheza nyuma ya mshambuliaji.
Ubunifu wake ulimfanya kumudu kucheza maeneo hayo, lakini chini ya benchi la ufundi la sasa, Chama ambaye alionekana kupungua makali, ameonekana kurejea huku akitumika zaidi katika eneo la kiungo la ndani.

Katika mchezo wa kwanza chini ya Vandenbroeck ambao ulikuwa dhidi ya Arusha FC katika Kombe la FA ni Chama na Ibrahim Ajibu ambao walicheza katika eneo la juu la kiungo huku chini akicheza Mbrazil, Gerson Fraga na katika maeneo ya pembeni wakicheza, Deo Kanda na Francis Kahata anayeonekana kuwa katika kiwango bora.

Alikuwa huru, Chama kuzunguka katika eneo hilo huku akionekana kuwa hatari zaidi, alifunga katika mchezo huo na kuisaidia Simba kuibuka na ushindi wa mabao 6-0.
Katika mchezo wa pili ambao ulikuwa dhidi ya Lipuli katika Ligi, Chama aliendelea kutesa katika mfumo wa 4-5-1 kwa kucheza na Sharaf Shiboub katika eneo la kiungo la juu huku chini akicheza Jonas Mkude katika maeneo ya pembeni walicheza Kahata na Dilunga.
Chama hakufunga lakini alionekana kuwa mchango katika mchezo huo ambao waliibuka na ushindi wa mabao 4-0.

MSIKIE CHAMA
Akizungumzia vile ambavyo anatumika kwa sasa, Chama alisema, “Sio eneo geni kwangu kwa sababu hata mwanzo nilikuwa nikizunguka kote hata kama nilikuwa nikitokea pembeni. Naamini tutakuwa na msimu mzuri, kikubwa ni kuendelea kucheza kwa kushirikiana kama timu.”
Huu ni msimu wa pili kwa Chama kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara. Ndani ya msimu wake wa kwanza aliisaidia pia Simba kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo waliondolewa na TP Mazembe.

SIMBA WA YUDA
ANANGURUMA
Kaimu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Mwina Kaduguda ‘Simba wa Yuda’ alisema kwa ubora wa kikosi chao wanachowaza zaidi ni kukijenga kwa ajili ya mashindano ya kimataifa kuchukua Ligi kwao sio jambo la kujadiliana.
“Hatuna mawazo na Yanga, sio saizi yetu, ushiriki wetu katika Ligi ni kuchukua ubingwa ili turejee katika mashindano ya kimataifa,” alisema.
Msimu huu, Simba waliishia raundi ya awali kwa kuondolea katika Ligi ya Mabingwa Afrika na UD Songo ya Msumbiji kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya jijini hapa kutoka nao sare ya bao 1-1 huku katika mchezo wa kwanza, walitoshana nguvu kwa kutoka suluhu nchini Msumbaji.
Simba imedhamiria kufika mbali msimu ujao.

Post a Comment

0 Comments