NA SALEH ALLY
MPIRA una mambo yake unayotaka wenyewe, kama ukienda tofauti basi na wenyewe unakuonyesha mambo hayako sawasawa.
Nasema hivyo kwa kuwa watu wengi ambao wamekuwa wakifanya isivyo sahihi, mara nyingi mpira unawapa majibu kulingana na kile ambacho kipo sahihi.
Mfano, mchezaji nyota ambaye ana uhakika wa namba katika kikosi anachokitumikia. Halafu anaanza mambo ya starehe, upungufu wa nidhamu na kadhalika. Lazima atapata majibu yanayofanana na anachokifanya.
Mara zote, majibu ya tabia hizi huwa ni kufeli na mwisho wengi wamekuwa wakitumbukia shimoni kabisa kwa kuwa hawapendi kukubali kwamba kweli wamekosea kulingana na kinachoendelea.
Kama mchezaji atakuwa anajituma, ana nidhamu na msikivu kufuata maelekezo ya makocha wake na anashirikiana na wenzake, jibu lake huwa ni mafanikio tena kwa haraka.
Mfano mzuri ni beki namba mbili wa Yanga, Paul Godfrey, maarufu kama Boxer. Angalia namna alivyokatiza katika msitu wa ufalme wa Juma Abdul na kufikia alipo sasa.
Boxer sasa ni kati ya wachezaji gumzo katika Ligi Kuu Bara. Hakika ameonyesha ni mwenye nia ya kufanya vema na anaweza kutengeneza mwendelezo wa kufanya vizuri zaidi.
Beki huyo wa kulia wa Yanga, kama ataendelea na mwenendo wa sasa wa kucheza kwa kujituma basi atakuwa tegemeo si Yanga pekee, badala yake hata kwa taifa letu nafasi ambayo anastahili baada ya miezi michache ijayo kama atakuwa na mwendelezo huu.
Kijana huyo anajituma sana, uchezaji wake ni direct football. Yaani mtu anayecheza kusukuma timu kwa lengo la ushindi na kadhalika katika ulinzi ni kupambana na kuhakikisha kikosi hakipotezi mchezo.
Ana kazi ya kupandisha mashambulizi na anakuwa beki wa pembeni hatari kwa mabeki wa bembeni wa timu pinzani.
Kwa mfumo wa soka la kisasa, mabeki wa pembeni wamekuwa kati ya wachezaji ambao wanauzwa kwa bei kubwa kwa vile wanatumika sana katika upangaji mashambulizi pia ulinzi.
Hivyo timu nyingi ili zifanye vizuri zinahitaji mabeki bora wa pembeni kufanya vizuri katika michuano mbalimbali zinazoshiriki.
Kama unaona Juma Abdul anakaa nje na mechi inapoisha hauwezi kumuulizia yuko wapi au anaendeleaje, basi ujue ubora wake uko katika kiwango sahihi.
Boxer anaweza sasa kuchagua njia, kuendelea na alichokianzisha au kupishana nacho. Na tukubaliane, sisi kwa kuwa tunafurahishwa na kazi yake, basi tuna kila sababu ya kusema ikiwezekana kusifia.
Huu ndio utaratibu sahihi wa kuwa muwazi, ukifanya vema vizuri tuseme ukfanya vibaya, basi kuwe na nafasi ya kusema ukweli na kuuelezea mwenendo wako kwamba si mzuri au unavurunda.
Boxer ndio ameanza kuchipukia kikazi, maana yake ana safari ndefu kwa kuwa soka linatoa nafasi kwa wanaofanya sahihi tena na tena, tena na tena.
Soka halitoi nafasi kwa wanaofanya vizuri leo na kesho wanavurunda kwa kisingizio kwamba walifanya vema jana au juzi.
Hivyo Boxer ana mzigo ambao dalili zinaonyesha anauweza lakini pia inawezekana utamshinda kama hatakuwa makini kwa kuwa wako wanaoweza kumharibia na starehe ni namba moja.
Starehe haziji zenyewe, zinaambatana na watu ambao wanapitia watu ambao wanakuwa wanazileta hizo starehe kama sehemu ya kumshukuru au kumpongeza Boxer kwa kazi nzuri.
Boxer kuwa makini, usikubali kuingia katika mtego huo ambao umewaondoa wengi njiani na leo wanapambana kurejea lakini kazi ni ngumu.
Ukiona wanaotaka kukuangusha wanataka kukupongeza kwa pombe (kama unakunywa) au wanawake, kataa kwa kuwa pongezi yako ni ushindi wa makombe kwa timu unazozitumikia.
0 Comments