Windows

MDADA HUYU MBONGO APASUA ANGA KIMATAIFA MPAKA IKULU YA MAREKANI


UNAMKUMBUKA yule mdada ambaye alipata umaarufu kwa kupiga danadana na kuuchezea mpira? Habari ni kuwa uwezo wake huo umevuka mipaka kiasi cha kufika mpaka kwa mkuu wa nchi ya Marekani.

Binti huyo ambaye jina lake halisi ni Hadhara Charles, alipata umaarufu kwa kuonyesha uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira kuliko hata wachezaji wengi wanaume wa mchezo huo, ambapo mara kadhaa amewahi kutumika kutoa shoo kwenye matukio mbalimbali ikiwemo yale ya Uwanja wa Taifa.

Kusambaa kwa video zake akiwa katika kazi yake hiyo ambayo imekuwa ikimpatia kipato ni kawaida, watu wa nchi mbalimbali wamekuwa wakiona uwezo wake na kumsifia lakini safari hii Rais wa Marekani, Donald Trump naye ameona na kutoa neno.

Trump ambaye ni kawaida yake kutoa matamko na maoni mbalimbali kupitia ukurasa wake wa Twitter, safari hii aliutumia pia kuelezea hisia zake juu ya binti huyo Mtanzania ambaye amekuwa akitoa burudani katika nchi mbalimbali.


Siku kadhaa zilizopita ndani ya mwezi huu wa pili, kuna video kadhaa za Hadhara zilikuwa zikisambaa mitandaoni na watu mbalimbali kutoa maoni huku wengi wakitaja kuwa binti huyo anatokea mataifa yao mbalimbali ya Afrika.

Ndipo mtumiaji mmoja kwa jina la Akin Sawyerr akaiposti video ya Hadhara akionyesha ujuzi wake mbele ya watu huku wakimshangilia.


Hadhara alikuwa amezungukwa na wanaume mbalimbali ambao walikuwa wakizungumza na kushangilia kwa kuona yale aliyokuwa akiyafanya. Muda mfupi baada ya kuwekwa kwa video hiyo, ndipo Trump akaiona na kuamua kutoa neno na kui ‘retweet’, yaani kuweka neno kisha inatokea kwenye ukurasa wake yeye Trump. 

Trump aliamua kuandika neno moja tu: “Amazing!” akimaanisha kitu kizuri ambacho kimemshangaza.

Video hiyo yenye sekunde 84, ikaanza kusambaa kwa kasi kwa watu mbalimbali kutoa maoni ambapo hadi jana kulikuwa na maoni zaidi ya 9,000 kwenye ukurasa wa Trump.

Licha ya kuwa watoa maoni wengi hawakujua Hadhara ni nani na anatokea nchi gani hasa, lakini bado walikuwa wakisifia na kueleza kuwa anatokea Afrika. Katika video hiyo, Hadhara anaonyesha umaridadi wa kumiliki mpira kwa kuupiga kwa kichwa mara nyingi, mabegani, mgongoni na kuutuliza kifuani.

Sifa zilikuwa nyingi na maoni mengi yalikuwa yakimsifia na kusema kuwa amekuwa bora katika kumiliki mpira na kuuchezea kuliko hata ilivyokuwa wakati Ousmane Dembele alipokuwa akitambulishwa kujiunga na Barcelona ya Hispania mwaka 2017.

Maoni mengi yaliendana na video ya Dembele alipokuwa akitaka kupiga danadana lakini mpira ukawa unaenda pembeni, alifanya hivyo lakini hakufanikiwa, licha ya kuwa alikuwa amenunuliwa kwa fedha nyingi. Maoni mengine yalieleza kuwa licha ya kuwa na kipaji cha juu lakini mazingira ya binti huyo yalionyesha wazi kuwa hakuwa mtu mwenye kipato kikubwa kwa kuwa hata mavazi yake yalikuwa ya kawaida na yanaonyesha ni mtu wa kipato cha chini.

V i d e o hiyo ya Hadhara ambayo imetazamwa zaidi ya mara milioni 10, pia upande mwingine ilikuwa mwiba k w a R a i s Trump kutokana na kurushiwa maneno makali na baadhi ya watoa maoni hasa wa Marekani.

Maoni ya kumkosoa Trump yalitolewa kutokana na kile kilichoonekana kuwa anaacha kuangalia au kuzungumzia mambo ya ‘kawaida’ na ambayo hayamuhusu. Suala la mpaka wa Marekani na Mexico uliingilia kati mjadala huo kwa kumwambia kuwa Trump anatakiwa kuzungumzia matukio kama hayo na siyo kuangalia video za soka ambazo hazimuhusu.

Mmoja wa wachangiaji mada alisema: “Anatakiwa kuwa kwenye kazi za kuiendesha nchi na siyo kuanza kushea video katika mitandao ya kijamii kama kijana mdogo.” Pamoja na hivyo, bado kulikuwa na wafuasi wa Twitter ambao walionyesha kumuunga mkono na kumsapoti kwa kile alichokifanya wakisema naye ni binadamu ana masuala yake binafsi na hawezi kupangiwa kila kitu cha kupenda na kuzungumzia.


Post a Comment

0 Comments