Azam haijapata matokeo mazuri katika michezo yake miwili mfululizo ilianza kutoka sare ya mabao 2-2 na JKT Tanzania kisha ikachapwa bao 1-0 na Coastal, hivyo kocha msaidizi wa kikosi hicho, Idd Nassor ‘Cheche’ amesema sasa imetosha.
KIPIGO ilichopewa na Coastal Union na ushindi wa Yanga dhidi ya Prisons imeifanya Azam iporomoke kwa nafasi moja kutoka ya tatu hadi ya nne, jambo ambalo limewafanya mamocha wa timu hiyo kushtuka na kuwaambia vijana wao, lazima wakaze mbele ya Polisi Tanzania.
Azam na Polisi jioni ya leo watavaana kwenye Uwanja wa Ushirika, mjini Moshi kila moja ikiwa na matokeo tofauti kwa mechi zao zilizopita za Ligi Kuu Bara, Wanalambalamba wakilala 1-0 jijini Tanga mbele ya Wagosi, wakati maafande wakitaka nyumbani dhidi ya KMC kwa kuichapa 2-1.
Kutokana na matokeo hayo, timu zote zimeupania mchezo wa leo, huku Azam wakisisitiza hawatakubali kulala tena ugenini, huku wenyeji wanaonolewa na Kocha Malale Hamsini wakisisitiza dozi inaendelea kama kawaida ili kuhakikisha wanamaliza msimu katika nafasi nzuri.
Azam haijapata matokeo mazuri katika michezo yake miwili mfululizo ilianza kutoka sare ya mabao 2-2 na JKT Tanzania kisha ikachapwa bao 1-0 na Coastal, hivyo kocha msaidizi wa kikosi hicho, Idd Nassor ‘Cheche’ amesema sasa imetosha.
Cheche alisema wameyafanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Coastal na wanaingia kuikabili Polisi Tanzania kwa nguvu zote kuhakikisha wanaondoka na pointi zote tatu.
“Tunaendelea na maandalizi na hapa tunajiandaa jioni (jana) tukafanye mazoezi ya mwisho ili kurekebisha baadhi ya makosa kwani kama unavyojua hatukuwa na matokeo mazuri katika mchezo uliopita, lazima turekebishe mambo kusudi twende vizuri katika mchezo dhidi ya Polisi,” alisema.
“Polisi Tanzania ni wazuri na tunawaheshimu, na tunajua wako nyumbani, lakini tutahakikisha tunapambana kwa hali zote ili tuweze kupata matokeo mazuri,” aliongeza Cheche.
Naye Kocha wa Polisi, Malale alisema mchezo huo uitakuwa mgumu kwani wanakutana na timu nzuri Azam ambayo imetoka kupoteza mchezo hivi karibuni.
“Tunajua tunakutana na timu iliyotoka kupoteza mechi hivyo watakuja kwetu wakihitaji kupata matokeo mazuri kupitia sisi. Tunajua itakuwa mechi yenye ushindani mkubwa lakini tumejipanga kuwakabili kwani hata sisi pia tunataka pointi tatu.
“Mechi iliyopita tulishinda, hivyo hatutaki kupoteza dhidi ya Azam ukizingatia tutakuwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani,” alisema Malale ambaye atawakosa wachezaji wawili leo, Juma Kikuti aliyeshikwa na homa na Rashid Mustapha mwenye matatizo ya goti.
Mbali na mchezo huo, jijini Dar es Salaam nako kutakuwa na kitupe kingine, maafande wa JKT Tanzania watakuwa wenyeji wa Namungo FC kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Kocha wa Namungo, Hitimana Thierry amekiri matokeo yao katika mechi tano zilizopita hayakuwa mazuri baada ya kushinda mechi mbili tu na kupoteza tatu hivyo lazima wakomae katika mchezo wa leo dhidi ya JKT Tanzania ili washinde.
“Ingawa tuko nafasi ya 10 katika msimamo lakini bado hatuko vizuri tunahitaji kuongeza bidii na kushinda mechi zetu zinazofuata, kwani tumekuwa na matokeo mabovu kwa mechi za ugenini, lakini tumejipanga kufanya vizuri mbele ya JKT ambao sio timu ya kubezwa,” alisema Hitimana.
Kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed ‘Bares’ atakayemkosa beki wake kisiki Adeyum Saleh aliyesajiliwa na Yanga katika dirisha hili la uhamisho, alisema wamejipanga kupata matokeo mazuri nyumbani, licha ya kukiri Namungo ni wazuri.
0 Comments