Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa amesema hawana hofu kuelekea mchezo dhidi ya Simba utakaopigwa January 04 2020 kwenye uwanja wa Taifa
Mkwasa aliyewahi kuwa dimbani kwenye mchezo wa watani akiwa mchezaji na baadae kocha, amesema Simba ni timu ya kawaida
Mkwasa amesema kwa sasa wameweka nguvu kwenye mechi za viporo ambazo watacheza kabla ya mchezo huo
"Ni mapema sana kuzungumzia mchezo dhidi ya Simba Januari 04 kwani tuna mechi nyingine kabla ya mchezo huo"
"Lakini kwa ufupi niseme kuwa Simba ni timu ya kawaida kama zilivyo timu nyingine ambazo tayari tumecheza nazo," alisema Mkwasa
Kikosi kimeiva
Katika hatua nyingine, Mkwasa amesema vijana wake wameanza kufanyia kazi mafunzo ambayo amekuwa akiwapa mazoezi na hivyo kuiongezea timu makali hasa katika ushambuliaji
"Kwa sasa vijana wanaelekea vizuri kwani wanayafanyia kazi yale ambayo tumekuwa tukiyafanya mazoezini. Unaona sasa wanatengeneza nafasi nyingi na kuzitumia baadhi kufunga mabao. Mwanzoni hali ilikuwa tofauti"
"Ni mwelekea mzuri na inatoa picha nzuri kwani naamini kwenye mechi zijazo tutaweza kufanya vizuri zaidi kuliko sasa," alisema
Katika mchezo wa kombe la FA uliopigwa jana dhidi ya Iringa United, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-0
Kwenye mchezo huo Mkwasa aliwakosa nyota saba waliokuwa timu za Taifa za Zanzibar na Tanzania Bara ambao wamerejea hivi karibuni kutoka nchini Uganda walikokwenda kushiriki michuano ya Chalenji
Lakini pia aliwakosa nyota wake wapya Tariq Seif, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima na Adeyum Saleh ambao mchakato wa usajili wao haukuwa umekamilika
0 Comments