Windows

Katwila aongeza nguvu Stars



KOCHA wa Mtibwa, Sugar Zuberi Katwila ameongezwa kwenye benchi la ufundi la timu ya soka ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kuungana na makocha Juma Mgunda na Selemani Matola kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Chalenji.

Michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) inatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii ambapo Stars itaanza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Zanzibar Heroes.

Katwila ndiye kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, iliyotwaa ubingwa wa Chalenji kwa wachezaji wa umri huo miezi michache iliyopita, pia ni kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20.

Akizungumza na gazeti hili jana kwenye mazoezi ya Stars kuhusu ujio wa kocha huyo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo alisema Katwila amejiunga na Stars ili kupata uzoefu kwani yeye ni kocha wa timu za taifa za vijana.

“Katwila ameongezwa kwa ajili ya kuja kupata uzoefu kusaidiana na Mgunda (Juma) pamoja na Matola (Selemani) ikiwa ni sehemu ya yeye kujifunza zaidi,”alisema.

Kocha huyo alionekana jana kwenye mazoezi ya Stars akiwa na wenzake wakijiandaa kwa maandalizi ya michuano hiyo. Kilimanjaro Stars inatarajiwa kuondoka kesho kuelekea Uganda tayari kwa michuano hiyo.

Kwa mujibu wa Ndimbo kila kitu kiko sawa na wachezaji wa kimataifa wameanza kuwasili. Golikipa wa Gor Mahia, David Kisu aliwasili jana asubuhi na kujiunga na wenzake huku wengine watatu wakiwemo Eliud Ambokile kutoka TP Mazembe, Eliuta Mpepo kutoka Buildcon Zambia na Dikson Kibabage wa Difaa El Jadida ya Morocco wakitarajiwa kujiunga na wenzao wakati wowote.

Aidha, baadhi ya wachezaji hawakuonekana mazoezini wakiwemo Abubakari Salum huku Ndimbo akisema alifika asubuhi kueleza kuwa aliumia mchezo uliopita. Mwingine ni Kelvin Yondani ambaye Ndimbo alisema hajapata taarifa zake.






Post a Comment

0 Comments