

Mshambuliaji hatari wa Simba Meddie Kagere 'Mk14' ametaja sababu iliyofanya kasi yake ya kufunga mabao aliyoanza nayo mwanzoni mwa msimu kupungua
Katika michezo sita ya mwanzo msimu huu Kagere alifunga mabao saba lakini kwenye michezo minne iliyofuata mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Rwanda alipachika bao moja tu
Kagere amesema moja ya sababu zilizofanya apungue ubora ni kutokuwa na muda wa kupumzika
"Nimecheza mechi zote za Simba na Rwanda kwa dakika 90, ninakosa muda wa kutosha wa kupumzika na kujifanyia tathmini," amesema
"Lakini pia mafanikio ambayo nimeyapata yamefanya kuwa mchezaji ambaye nalindwa zaidi na timu pinzani. Nalazimika kupambana zaidi ili kuweza kufunga na hata kama sifungi basi niwatengenezee wenzangu wafunge"
"Changamoto nyingine ni za kibinadamu, naweza kupanda na kushuka kiwango kwa nyakati tofauti. Muhimu nachukulia hii kama changamoto na naamini nitarejea kwenye ubora wangu muda sio mrefu"
Kagere anaendelea kuongoza orodha ya vinara wa mabao ligi kuu msimu huu akiwa amefunga mabao 8
Anafuatiwa na Paul Nonga wa Lipuli mwenye mabao saba huku Miraji Athumani na Daruweshi Saliboko wakiwa na mabao sita kila mmoja
Kwa habari zaidi Download App ya soka kiganjani kutoka Play Store.



0 Comments