Windows

Aishi Manula : Nakosa muda mwingi wa kuihudumia ndoa yangu


WAHENGA wanasema utamu wa ngoma uingie ucheze mwenyewe, hivyo hivyo raha na karaha ya mapenzi anayajua ni yule ambaye yupo kwenye uhusiano husika.




Wakati wengine wanapambana kuumizwa na mapenzi huku wengine wakiamini mambo hayawezi kwenda kutokana na kuingia katika mapenzi na kujikuta wakishindwa kufikia malengo waliyokusudia.


Asikuambie mtu kipenda roho hula nyama mbichi, muulize Aishi Manula atakuambia uhalisia wa msemo huo baada ya kuingia kwenye ndoa na Aisha Thabiti ambaye ni mke halali wa ndoa aliyefunga naye ndoa mwanzoni mwa mwaka huu.


Manula ambaye ni kipa namba moja wa Simba anajua raha na si karaha katika mapenzi kutokana na kuthibitisha kuwa akipenda anapenda kweli.


KINARA WA MAPENZI


Wakati wengine wakiamini msemo wa mapenzi yanauma kutokana na kuumizwa nayo, basi kuna wengine wanayachukulia kama kutafuna Big G kutokana na kuyaweza na kuendanayo sawa, hivyo ndivyo ilivyo kwa Manula.“Kwenye mahusiano sijawahi kutendwa, hiyo ni kutokana na kuwa mwaminifu na naamini katika kuaminiana hiyo inaweza ikawa siri ya mafanikio katika mahusiano yangu,” anasema nakuongeza kuwa:


“Nipo katika ndoa na ninapendana na mke wangu mahusiano yetu ni ya muda mrefu hadi kufikia hatua ya kuwa mke na mume lakini hadi sasa tangu tumeoana hatujabahatika kupata mtoto,” anafunguka.


HAFURAHII NDOA


Wakati akibainisha kuwa tangu ameanza uhusiano hajawahi kutendwa kutokana na mahaba aliyonayo kwa mke wake tangu enzi wakiwa ni wapenzi kipa huyo anabainisha hajawahi kufurahia ndoa yake.


“Sina maana kwamba hatupendani au hanilidhishi hapana sifurahii kwasababu sina muda mwingi wa kukaa na familia yangu, muda mwingi nautumia katika kazi zangu kitu ambacho sio kizuri kwangu na familia yangu nikiwa na maana mke,” anasema na kuongeza:


“Mara nyingi tukiwa kambini huwa nakuwa mwenyewe mke huwa namuacha nyumbani na kambini tunaweza kukaa hata mwezi au hata wiki mbili sasa nasemaje ndoa nimeifuraia ndo kweli?” Anahoji.


MASHABIKI WANAMJENGA


Hakuna ubishi kuwa mkusanyiko wa watu wengi katika mazingira yoyote lazima utakuwa na changamoto ambazo kunakuwa na za kuelimisha, kukosoa, kuburudisha na kufundisha.


Hilo limethibitishwa na Manura ambaye amefunguka kuwa kazi yake anayoifanya inampa changamoto hasa kwenye mkusanyiko wa watu ambao muda wowote wanaweza kumkatisha tamaa kama ataamua kwenda na upepo wa mawazo yao.


“Ni kweli kuna wakati ukiwa uwanjani unaweza kusikia maneno mazito kutoka kwa mashabiki wa timu pinzani, na kama ukiwa na roho nyepesi yanaweza kukutoa kwenye mood na hiyo ndiyo dhamira yao, kikubwa ukiyazoea unaona kawaida tu,” anasema.


ALIKIBA, DIAMOND FRESH


Kila binadamu ana starehe yake kuna wanaopenda mpira nikiwa na maana kuangalia, wengine filamu, mieleka, mpira wa kikapu na wengine muziki ndio kila kitu wakisikiliza wanaondoa mawazo.


“Napenda kucheza soka kwasababu ndio majukumu yangu lakini sio kwamba muda wote nitakuwa katika majukumu hayo, hivyo muda wangu wa mapumziko nimekuwa nikisikiliza muziki ili kuweza kupumzisha akili,” anasema na kuongeza:


“Huwa nasikiliza sana muziki nikiwa kambini, na mara chache nikiwa nyumbani sina msanii maalumu wa kumsikiliza nyimbo yoyote yenye kuburudisha huwa naisikiliza innaweza kuwa ya Alikiba au Diamond ili mladi tu ananiburudisha huwa ninaisikiliza,” anasema Manura.


Post a Comment

0 Comments