

Beki wa pembeni wa Simba Gadiel Michael amesema msimu huu anakabiliwa na ushindani mkali wa namba ndani ya kikosi cha Simba
Gadiel aliyetua Simba mwanzoni mwa msimu akitokea klabu ya Yanga, kwa siku za karibuni amekuwa na wakati mgumu kupata namba mbele na Mohammed Hussein 'Tshabalala' ambaye amekuwa na kiwango kizuri tangu apone majeraha
'Battle' ya Gadiel na Tshabalala haiko Simba tu, ni mpaka timu ya Taifa kwani walinzi hao ndio wanaotegemewa huko pia
Gadiel amesema ushindani huo unamfanya ajitume zaidi
"Asikuambie mtu ligi ni ngumu hii inasaidia mchezaji kujituma kwa bidii kufanya kazi yake kuhakikisha hawaangushi waliomwajiri," amesema
"Lengo langu ni kuhakikisha nakuwa na mchango mkubwa Simba ambao wamenipa ajira na kuniamini kwamba nitaweza kufanya maajabu"
"Nina ndoto za kufika mbali, huwa nafurahia kuona ninayeshindana naye kwenye namba anakuwa na kiwango kikubwa, kinachokuwa kinanifanya mimi kuwa makini zaidi"
Ushindani wa namba Simba hauko kwa Gadiel na Tshabalala tu, kwani Simba ilifanya usajili ambao umeifanya timu hiyo kuwa na wachezaji sio chini ya wawili wenye uwezo kwenye nafasi moja
Hii ndio sababu inayoifanya Simba kuonekana klabu iliyokamilika zaidi na kupewa nafasi ya kutetea ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems ana wigo mpana wa uchaguzi wa wachezaji katika kila mchezo
Mara kadhaa Aussems aliwaambia waandishi wa habari kuwa ana wachezaji 24 ambao anaweza kuwatumia sawa sawa



0 Comments