KUFUATIA Bodi ya Ligi Tanzania (TPBL) kumfungia mechi tatu Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera pamoja na kumpiga faini ya shilingi laki tano kutokana na makosa yaliyojitokeza katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting, uongozi wa klabu hiyo umeamua kutinga katika Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kuripoti madudu yanayofanyika kwenye ligi.
Bodi ya Ligi imemfungia mechi tatu Zahera kutokana na kosa la kuitolea maneno mabaya bodi hiyo ikiwa ni pamoja na kumpiga faini ya Sh 500,000 kutokana na kuvaa mavazi yasiyostahili katika mechi hiyo ya Ruvu hali ambayo uongozi wa klabu hiyo haukufurahishwa nao.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alinukuliwa akieleza juu ya mabadiliko ya baadhi ya kanuni za ligi likiwemo suala la benchi la ufundi kuwa katika mavazi rasmi ya pamoja ikiwemo kocha kuvaa mavazi nadhifu.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amefunguka kuwa, tayari wameshaitaarifu wizara husika juu ya madhaifu ambayo yanajitokeza ndani ya bodi ili kuweza kuchukua hatua.
“Bodi ilitakiwa imuite kwanza Zahera na kumueleza makosa yake, hawezi kuisema bodi kama hakuna jambo, busara inasema kama mtu anazungumzia jambo mwiteni mumsikilize, bodi siyo Mungu ni watu tu, kwa mfano timu inatoka Gaborone na kuwasili Jumatatu ikitokea kwenye mechi ngumu ya ubingwa wa Afrika, Jumanne kunakuwa hakuna mazoezi na Jumatano mechi, hivi kweli kocha asilisemee hilo!
“Unapomfungia mechi tatu kwa nini usimpe faini aendelee kuifundisha timu, tumeshaiambia wizara haya madhaifu na tunasubiri majibu, itafika mahali Wanayanga tutasema na tukisema tutamaanisha, utafika wakati nasema tutasema na tukiwa na jambo letu nina uhakika hakuna wa kutuzuia moto wetu sasa wakati unawadia,” alisema Mwakalebela.
TAIFA STARS Walivyotua BONGO Kwa SHANGWE, SAMATTA, MSUVA Wazungumza!
The post Yanga Yaijia Juu Bodi ya Ligi Kisa Zahera appeared first on Global Publishers.
0 Comments