Windows

Yanga Yaifuata Zesco Usiku Kibabe

MSAFARA wa wachezaji 21 wa Yanga unatarajiwa kusafiri kesho Jumanne saa 2:00 usiku kuwafuata wapinzani wao Zesco United watakaovaana Jumamosi hii.

 

Yanga itacheza na Zesco katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa huko Ndola, Zambia.

Katika mchezo wa awali uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema kuwa maandalizi ya timu hiyo yanaendelea vizuri na kesho saa mbili usiku itasafiri kwa ndege kuelekea Ndola, Zambia.

 

Saleh alisema kuwa katika msafara huo wachezaji wanne pekee ndiyo watakaowaacha ambao ni Paul Godfrey ‘Boxer’, Issa Bigirimana ‘Walcott’ wenye majeraha, wengine ni David Molinga ‘Falcao’ na Selemani Moustafa ambao bado hawajapata vibali. Aliongeza kuwa wachezaji Falcao na Moustafa bado uongozi unafanya jitihada za kutosha kuhakikisha wanapata vibali vyao ili washiriki michuano hiyo mikubwa Afrika.

 

“Maandalizi ya safari yamekamilika kwa kiasi kikubwa na msafara wa timu unatarajiwa kuelekea Zambia keshokutwa (kesho) saa mbili usiku.

 

“Tumepanga kuwahi kufika Zambia kwa ajili ya wachezaji kuzoea mazingira ya huko kabla ya mchezo wetu na uzuri tayari baadhi ya viongozi wamefika huko kwa lengo la kuandaa kambi.

 

“Katika msafara wetu watakosekana wachezaji wanne, kati ya hao wawili ni majeruhi ambao ni Boxer, Bigirimana na wengine bado hawajapata vibali, nao ni Falcao na Moustafa,” alisema Saleh.

 

Naye mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla amesema watakwenda nchini humo na mahitaji yao yote muhimu ikiwemo chakula na maji.

 

“Tunatazama uwezekano wa kubeba chakula chetu pamoja na maji kwa lengo la kuepuka usumbufu wa mahitaji hayo pindi tutakapokuwa Zambia, kama tunavyofahamu mechi zetu za Afrika huwa na figisu figisu nyingi, hivyo hatutaki kuyumba na ndiyo maana tunataka kwenda Zambia tukiwa kamili,” alisema Msolla.

The post Yanga Yaifuata Zesco Usiku Kibabe appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments