Windows

Mzungu Amtengenezea Straika Mbrazili Kombinesheni Hatari

STRAIKA mpya wa Simba, Mbrazili, Wilker Henrique Da Silva, rasmi ataanza kutumika kwenye michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara na tayari Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems ameanza kwa kumtengenezea kombinesheni mbili.

 

Mbrazili huyo alirejea uwanjani wiki iliyopita kufanya mazoezi ya pamoja baada ya kupona majeraha ya goti yaliyomuweka nje kwa mwezi mmoja na nusu, hivyo mashabiki bado hawajafanikiwa kuona makeke yake uwanjani.

 

Straika huyo juzi alifanikiwa kufunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 3-0 walioupata katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Azam FC U20 Uwanja wa Gymkhana jijini Dar es Salaam.

 

Straika huyo alionekana kupangwa kucheza na wachezaji wawili tofauti katika mchezo huo wa kirafiki baada ya awali kupangwa na Msudan, Sharraf Eldin El Shiboub aliyecheza namba 10 kama kiungo mchezeshaji huku Mbrazili huyo akipangwa 9.

 

Wakati mechi hiyo inaendelea, Shiboub na Wilker walionekana kucheza kwa kuelewana huku wakitengenezeana nafasi za kufunga mabao.

Wakati wakitengenezeana nafasi hizo, Shiboub ndiye aliyefunga bao la kwanza akiitumia vema pasi ya Francis Kahata kabla ya Wilker kupachika mawili huku moja akitumia krosi safi ya Shiboub.

 

Katika kipindi cha pili, kocha huyo alimbadili Shiboub kwa kumrudisha namba nane na kumhamishia kiungo fundi Mzambia, Francis Kahata namba 10 ambaye alicheza pamoja na Wilker.

Mara baada ya Chama kubadilishwa dakika chache baadaye, alimtengenezea bao Wilker kwa kumpa pasi safi kabla ya Mbrazili huyo kumchambua kipa wa Azam akiwa ndani ya 18 ya goli la wapinzani.

 

Mbelgiji huyo hakuwachezesha mastraika John Bocco na Meddie Kagere kwa kuwa ni majeruhi lakini Kagere ana nafuu na anaweza kuonekana uwanjani hivi karibuni.

Ikiwa washambuliaji wote hao watarejea, Aussems atakuwa na kazi ngumu ya kuchagua kikosi chake cha kwanza.

Mbrazili huyu bado watu hawajaona uwezo wake kwani amekuwa nje ya uwanja tangu msimu umeanza.

 

Alishiriki maandalizi ya msimu mpya, akacheza mechi moja ya kirafiki Afrika Kusini na kufunga bao moja kabla ya kuumia. Mechi ya juzi dhidi ya Azam U20 ndo ilikuwa ya pili kwake. Hajafanikiwa kucheza mechi yoyote ya kimashindano, hivyo Wanasimba wana shauku kubwa ya kuona uwezo wake.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

The post Mzungu Amtengenezea Straika Mbrazili Kombinesheni Hatari appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments