KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amefunguka wazi kwamba anaelewa kabisa kuwa kushinda kwenye Uwanja wa Kaitaba ni ngumu kutokana na matokeo mabaya ambayo wamekuwa wakiyaambulia uwanjani hapo, lakini atatumia nguvu kuhakikisha wanashinda.
Simba watasafiri kuelekea mkoani Kagera kwa ajili ya kucheza na Kagera Sugar kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo itapigwa Uwanja wa Kaitaba, Alhamisi ya wiki hii.
Msimu uliopita, Simba walishindwa kupata pointi uwanjani hapo baada ya kuchapwa mabao 2-1 huku pia wakichapwa 1-0 jijini Dar.
Aussems ameliambia Championi Jumatatu, kuwa amejipanga zaidi kwa kutaka kushinda kwenye uwanja huo licha ya kwamba ni ngumu kushinda uwanjani hapo.
“Najua ni ngumu kushinda kule Kagera kwa sababu katika misimu ya karibuni tulishindwa kupata matokeo pale. Lakini kwa safari hii tunataka kubadilisha kila kitu.
“Tunachotaka ni kuona tunashinda na kupata pointi japo haitakuwa rahisi hata kidogo, tunatakiwa kufanya kazi kubwa. Ninachokifanya ni kujiandaa kushinda safari hii na kuvunja tabia ya kutoshinda katika uwanja huo,” alisema Aussems.
Kwa upande wa kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula, alitamba kuwa wapo tayari kuvunja mwiko.
“Kwa msimu huu tunataka kuvunja mwiko mbele ya Kagera kwa kuona tunashinda na kuchukua pointi tatu mbele yao. Msimu uliopita tulishindwa baada ya kufungwa mechi zote mbili. Tutapambana kushinda na tunaamini tutalifanya hilo,” alisema Manula.
SAID ALLY, Dar es Salaam
The post Aussems: Kaitaba Kugumu, Tutashinda Kinguvu appeared first on Global Publishers.
0 Comments