MSHAMBULIAJI wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi, ndiye mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa kiume wa shirikisho la soka duniani (FIFA), maarufu kama ‘THE BEST’ akiwapiku Cristiano Ronaldo na Virgil van Dijk katika mtanange uliofanyika usiku wa Septemba 23 mjini Milan< Italia.
Siku chache baada ya kufanyika kwa tuzo hizo, baadhi ya manahodha na makocha wameibuka na kutoa malalamiko yao kuwa kura zao hazikuhesabiwa na hawakumpigia kura mshindi wa tuzo hiyo, Lionel Messi.
Miongoni mwa waliotoa malalamiko yao ni pamoja na shirikisho la soka la Misri na nahodha wa timu ya taifa ya Nicaragua, Juan Barrera, ambapo Misri ilihoji FIFA ni kwa nini kura za kocha wake Shawki Ghareeb na nahodha Ahmed Elmohamady hazikuhesabiwa na kwamba ilituma fomu yao Agosti 15 lakini FIFA haikujibu mpaka ilipofikia Agosti 21, hivyo kura zao kutohesabiwa.
FIFA imejibu malalamiko hayo ikisema kuwa fomu ya shirikisho la soka nchini Misri iliwasilishwa ikiwa haina saini ya katibu mkuu wa shirikisho, jambo ambalo ni la lazima.
Pia imejibu tuhuma za nahodha wa Nicaragua, Juan Barrera pamoja na kocha wa Sudan, Zdravko Logarusic, kuwa hawakumpigia kura Lionel Messi, ambapo kocha wa Sudan akisema kuwa aliwapigia kura Salah, Mane na Kylian wakati FIFA ikisema kuwa kocha huyo aliwapigia kura, Messi, Van Dijk na Mane.
“Tumepitia fomu zote zilizowasilishwa na mashirikisho ya soka ya Sudan na Nicaragua na nyaraka zote zimesainiwa na kuthibitishwa na mihuri sahihi ya mashirikisho hayo ya soka,” amesema msemaji wa FIFA.
The post Messi Aiponza FIFA, Nchi Tatu Zasema ‘Hatukumpigia Kura’ appeared first on Global Publishers.
0 Comments