Windows

Kamusoko azua hofu Yanga

WAKATI kikosi cha Yanga kikitarajia kuondoka kesho Jumanne kwenda nchini Zambia kupambana na Zesco United katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, mashabiki wamepata hofu.

 

Hofu ya kutofanya vizuri katika mchezo huo imeanza kuwakumba baadhi ya mashabiki wa timu hiyo mara tu baada ya kusikia kuwa mfungaji wa bao la Zesco United katika mchezo wa kwanza wa ligi hiyo uliochezwa Dar es Salaam, Thabani Kamusoko juzi Jumamosi kaifungia tena timu yake hiyo kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Zambia.

 

Bao hilo alilifunga dhidi ya Lumwana Radiants na kuiwezesha Zesco United kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

 

Kutokana na hali hiyo, kipa wa zamani wa Yanga, Ivo Mapunda, ameingiwa na hofu ya timu hiyo kufanya vibaya katika mchezo wake wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi hii.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mapunda alisema kuwa uwezo wa juu ambao Kamusoko amekuwa akiuonyesha uwanjani tangu alipotua Zesco lakini pia bao la juzi aliloifungia timu yake hiyo kwa njia ya faulo aliyopiga na kwenda moja kwa moja wavuni, anaona unaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa Yanga kupata ushindi.

 

“Hofu yangu ipo kwa Kamusoko kwani hivi sasa uwezo wake upo juu na anatishia amani, bao aliloifungia timu yake jana (juzi) ilipokuwa ikicheza dhidi ya Lumwana Radiants lilikuwa bao zuri.

 

“Alifunga kwa mpira wa faulo ambao ulienda moja kwa moja wavuni, kwa hiyo Yanga wanatakiwa kuwa naye macho sana katika mchezo wa marudiano watakaocheza Jumamosi huko Zambia,” alisema Mapunda.

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam

The post Kamusoko azua hofu Yanga appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments