Wananchi wa Kijiji cha Mpwayungu kata ya Mpwayungu, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajengea miundombinu ya afya ambayo imesaidia kuboresha huduma za afya katika kijiji hicho.
Wakiongea wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya afya na hali ya utoaji wa huduma za afya katika kijiji hicho iliyofanywa na Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima wananchi hao wamesema, kabla ya kujengewa miundombinu ya afya hali ya utoaji wa huduma za afya ilikuwa mbaya kiasi ambacho walikuwa wakifuata huduma hiyo katika Hospitali ya Mvumi.
Akiongea kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Kituo cha Afya cha Mpwayungu Bw. Chibwele Magubika amesema, awali hali ya utoaji wa huduma za afya katika kituo hicho zilikuwa duni kiasi ya kwamba wananchi wengi walikuwa wakikimbilia kupata huduma hizo katika Hospitali ya Misheni Mvumi au Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Bw. Magubika ameishukuru Serikali kwa kujenga miundombinu ya afya na kuboresha huduma za afya kwa wananchi ila ameiomba Serikali ihakikishe huduma hizo zinaboreshwa na kwamba, watumishi wanakuwa na lugha nzuri kwa wateja na kufanya kazi kwa weledi ili wananchi wengi waweze kuvutiwa na utoaji wa huduma katika kituo hicho.
“Inasikitisha kuona Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya afya yakiwemo majengo mazuri makubwa na yenye kuvutia lakini baadhi ya watumishi bado wanakuwa na lugha chafu ambazo haziwavutii wananchi kuja kupata huduma kwenye vituo kama hivi” Amesema Magubika.
Ameendelea kufafanua kuwa kuna baadhi ya watumishi hapa ni watovu wa nidhamu, wana lugha chafu kabisa, hawana maadili katika utendaji kazi wao, wanalewa pombe, hawatoi huduma kwa wakati jambo ambalo linakatisha tamaa wananchi kufika kupata huduma.
Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mpwayungu Selemani Kibakaya amesema kuwa, huduma zikiboreshwa, watumishi wakafanya kazi kwa ushirikiano bila kutegeana itasaidia kupunguza changamoto mbalimbali zinazojitokeza ikiwemo ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Amewataka wafanyakazi kuhakikisha wanatoa huduma kwa wakati, kwa kuwajali wagonjwa ili kuweza kupunguza msongamano pamoja na wananchi kukaa muda mrefu kusubiri huduma za afya jambo ambalo linakatisha tamaa ya kupata huduma za afya.
Wakati huohuo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima amawaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa kero wanazopata wananchi wakati wa kufika kwenye vituo vya huduma kwa kuongea na wateja, viongozi wa serikali ya kijiji na Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Kituo wanaowawakilisha wananchi kwenye uongozi wa kituo.
Vilevile, Dkt, Gwajima amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanachukua hatua stahiki kwa wakati pale wanapopelekewa malalamiko siyo tena nao wanakaa miezi 6 bila kuchukua hatua kama ilivyotokea kituoni hapo.
Dkt Gwajima amesema, ukosefu wa hatua stahiki dhidi ya kero zinazoripotiwa na wananchi ndiyo mojawapo ya mambo yanayowakwaza wananchi na kuamua kutotumia vituo husika au kuamua wanavyoona wao inafaa.
“CHMT NA RHMT hakikisheni mnafuatilia na kusimamia utendaji kazi wa watumishi katika vituo vya kutolea huduma, kutoa msaada na ushauri wa kitaalamu pia, kusikiliza kero za wananchi dhidi ya huduma na katika kila jambo, kuchukua hatua stahiki kwa wakati na bila kuonea upande wowote ule. Msisubiri hadi Wizara itembelee ndiyo iibue hizi kero na nyie mpo huku.
Amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuhakikisha anafanyia kazi malalamiko ya wananchi na kuchukua hatua stahiki za kiutumishi dhidi ya mtumishi Claude Chilala ambaye anatuhumiwa na wananchi kukiuka maadili ya kiutumishi na kuwa kero sugu kwa wateja.
Dkt. Gwajima amewapongeza watumishi wengine ambao wananchi wamekiri kuwa hawana shida ukilinganisha na huyo anayelalamikiwa na kila mteja.
Aidha amewataka watumishi kutoiga tabia ambazo zinakiuka maadili ya utumishi wa umma na kwamba, washirikiane daima vinginevyo, mambo yakiharibika inaweza ikawa vigumu kutowajibika kwa namna moja au ingine.
0 Comments