

Waandishi wa Habari nchini wameaswa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo wakati wa kuandika na kuripoti habari zinazohusu Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa lengo la kuchochea ustawi wa wananchi wa nchi wanachama hasa fursa zilizopo.
Akizumzunza wakati akifunga mafunzo ya kundi la kwanza la waandishi wa habari watakaoripoti na kuandika habari za SADC leo mjini Morogoro Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Balozi Hebert Mrango amesema kuwa, kila mwandishi analojukumu la kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu jumuiya hiyo na kwa wakati ili waweze kutumia fursa ya soko lililopo katika nchi 16 wanachama.
“Nchi za SADC zina soko kubwa linaloweza kuchangia katika kukuza uchuni wa nchi wanachama hivyo hii fursa ya kujitangaza wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi wananchama na Serikali” Alisisitiza Balozi Mrango.
Akifafanua amesema kuwa nchi wanachama ikiwemo Tanzania zina fursa ya kutangaza bidhaa zinazozalisha hasa zinazotokana na sekta ya Kilimo na Viwanda ili kuchochea ukuaji wa sekta hizo .
Kwa upande wake mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustiono Tanzania (SAUT) Dkt. Kaanaeli Kaale amesema kuwa kila mwandishi wa habari analo jukumu la kuhakikisha kuwa mwenendo wake unaendana na taratibu zote zinazosimamia taaluma hiyo kwa maslahi ya nchi wanachama wa SADC.
“Habari zinazoandikwa na kuripotiwa zinapaswa kulenga kujenga SADC na Afrika kwa ujumla kwa kuzingatia usahihi, ukweli, kufanya uchunguzi na kujiandaa vyema wakati wa kufanya mahojiano na Viongozi mbalimbali watakaoshiriki mkutano wa 39 wa Wakuu wa nchi na Serikali za nchi wanachama,” Alisisitiza Dkt Kaale
Akifafanua amesema kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na uelewa kuhusu manufaa ya Jumuiya hiyo na mchango wake katika kuleta ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt Ayub Rioba amesema kuwa waandishi wa habari wanapaswa kujenga uelewa kuhusu masuala yanayogusa nchi wanachama wa SADC kwa maslahi ya wananchi.



0 Comments