Taasisi ya ‘Miraj Islamic Center’ imekabidhi msaada wa vitu mbali mbali vilivyotolewa na jumuiya ya 'Humanity without borders' ya Uingereza kwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa ajili ya kuimarisha ustawi wa jamii na taasisi za kijamii mkoani humo.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo yenye Makao makuu yake jijini Dar es Salam Sheikh Arif Yussuf Abdulrahman alimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud kontena lenye bidhaa mchanganyiko zinazokisiwa kuwa na thamani ya Paundi za Uingereza 40,000 sawa na zaidi ya shilingi milioni 120.
Sheikh Arif alieleza kuwa gharama hizo zinajumuisha gharama za usafirishaji na kuwashukuru wadau wote walioko nje ya nchi ambao walichangia upatikanaji wa msaada huo.
Alisema jumuiya yake kwa kushirikiana na jumuiya nyengine zinatoa huduma za kijamii na kiutu zikiwemo za afya, elimu na kusaidia watu wenye shida kama mayatima na wagonjwa katika maeneo mbali mbali ya Tanzania.
“Taasisi yetu ni jumuiya ya kujitolea na si ya kupata faida bali hufanya hivi kusauidia jamii na ndio maana hatukusita kufanya hivyo tulipoombwa”, alisema sheikh Arif.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo yaliyofanyika katika bandari ya Zanzibar, Mkuu wa mkoa Mjini Magharibi Mhe Ayoub Mohammed Mahmoud aliahidi kuwa msaada huo utawafikia walengwa kwa kuzingatia aina ya msaada na mahitaji taasisi kwa uadilifu wa hali ya juu.
“Katika mzigo huu kuna bidhaa za vyakula, dawa, vifaa vya skuli, mashine za kuchanganyia zege na kadhalika. Vyote hivi vina uhitaji mkubwa ambao utasaidia kupunguza mahitaji ya jamii katika sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii ambako kuna mahitaji makubwa”, alieleza Ayoub.
Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa msaada huo unatokana na mazungumzo yaliyofanywa kati ya uongozi wa mkoa huo na jumuiya ya Miraj ambayo iliahidi kutafuta misaada na kuzipongeza taasisi hizo kwa kutimiza ahadi hiyo.
Aidha aliwaomba kutosita kutafuta wahisani wengine watakaosaidia juhudi zinazofanywa na serikali ya Zanzibar ya kutatua kero na kuwaletea maendeleo wananchi wake jambo amablo linapaswa kuigwa na taasisi nyengine.
Aidha ayoub alieleza kuwa pamoja na kupokea msaada huo kutoka katika jumuiya hizo, aliishukuru serikali kuu kwa kutoa msamaha wa kodi kwa mzigo huo ambao uliingia nchini.
0 Comments